Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » Makunga, Kibanda washinda kesi ya uchochezi

Makunga, Kibanda washinda kesi ya uchochezi

Alisema hata mashahidi wa upande wa mashtaka waliiambia Mahakama hiyo kuwa hakuna kitu chochote wala madhara yaliyowahi kutokea kwenye majeshi yao ya ulinzi ambayo ndiyo yaliyokuwa walengwa wa makaa hayo

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewaachia huru Meneja Uendelezaji Biashara wa Kampuni ya Mwananchi Communications (MCL), Theophil Makunga, Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2006), Absalom Kibanda na Samson Mwigamba katika kesi ya makala ya uchochezi iliyokuwa ikiwakabili.
Makunga na wenzake hao, walikuwa wakikabiliwa na kesi ya uchochezi dhidi ya askari wa majeshi ya ulinzi na usalama kwa kuchapisha makala kwenye Gazeti la Tanzania Daima iliyokuwa ikidaiwa kuwa na maneno yaliyolenga kushawishi askari majeshi ya ulinzi ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo (KMKM), Polisi na Magereza wasiwatii viongozi wao.
Akitoa hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi, Waliarwande Lema alisema kwa mtu yeyote mwenye kutafakari kwa makini hawezi kuita makala hayo ya Novemba 30, 2012 yaliyoandikwa na Mwigamba kwenye gazeti hilo yakiwa na kichwa cha habari ‘Waraka maalumu kwa askari wote’ kuwa ni uchochezi.
Hakimu Lema alisema hayo baada ya kupitia ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na mashahidi watatu wa upande wa mashtaka ambao ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari (Maelezo-Usajili wa Magazeti), Raphael Hokororo, Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Magereza (ACP), George Mwambashi kutoka Kitengo cha Sheria cha kikosi hicho na Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), David Hizza.
Alisema kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi hao, upande wa mashtaka umeshindwa kueleza jinsi washtakiwa hao walivyoshiriki kwenye makala yanayodaiwa kuwa ni ya uchochezi na kwamba walishtakiwa kwa hisia ambazo haziwezi kumtia mtu hatiani.
Hakimu Lema alieleza kuwa sheria ya jinai haihusishi kampuni, bali mtu hivyo upande wa mashtaka ulipaswa kuithibitishia Mahakama namna washtakiwa hao kila mmoja kwa wakati wake, alivyoshiriki kutenda kosa hilo kwa kuwa walikuwa na watu wengi waliokuwa wakiwasaidia katika kazi zao.
Alisema ushahidi huo hakuonyesha wala kuunga mkono namna Kibanda au Makunga walivyohusika kuchapa au kuhariri makala hayo yanayodaiwa kuwa ya uchochezi na kwamba ushahidi huo pia haujaonyesha kuwa ni ya uchochezi.
Alisema hata mashahidi wa upande wa mashtaka waliiambia Mahakama hiyo kuwa hakuna kitu chochote wala madhara yaliyowahi kutokea kwenye majeshi yao ya ulinzi ambayo ndiyo yaliyokuwa walengwa wa makaa hayo.
Upande wa mashtaka ulidai kuwa makala hayo yalikuwa ya uchochezi na kuwa yaliwashawishi askari wasiwatii viongozi wao ukiegemea Kifungu cha 32 (1)(c) na Kifungu cha 31(1)(a) cha Sheria ya Magazeti ambacho kinasema endapo litatokea kosa kwenye gazeti, mtu yeyote aliyeandika, kuchapisha na kusambaza atakuwa ametenda kosa.
“Machapisho ya uchochezi ni lazima yaonyeshe athari au madhara kwa kuleta uvunjifu wa amani, chuki, uhasama...” alisema Hakimu Lema.
Alisema SSP Hizza alikuwa mpelelezi wa kesi hiyo na mlalamikaji lakini katika ushahidi na hata uchunguzi wake, hakuwahi kuiambia Mahakama jinsi ambavyo kila mshtakiwa alivyohusika na kwamba Hokororo aliona hakuna tatizo lolote kwenye makala hayo ndiyo maana hakuchukua hatua yoyote dhidi yao.
Hakimu Lema alisema makala hayo hayakuwa na kitu chochote cha ajabu na kwamba Mwigamba alikuwa akijaribu kutumia haki yake ya kikatiba ya uhuru wa kujieleza na huku akisisitiza kuwa hayakuwa na nia ovu, bali maelezo binafsi na kuongeza kuwa upande wa mashtaka uliifungua kesi hiyo kwa hisia.
Alisema wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, SSP Hizza alimhoji mhariri lakini hakupeleka mahojiano hayo mahakamani kama kielelezo cha ushahidi.
Kwa upande wa ushahidi wa mshtakiwa Mwigamba, Hakimu Lema alisema ushahidi unaonyesha kwamba aliandika makala hayo kutokana na tukio la vurugu zilizotokea mkoani Arusha na kusababisha vifo vya watu watatu.
Alisema ili makala yathibitike kuwa ya uchochezi ni lazima kuwepo ama chuki au uvunjifu wa amani mambo ambayo hayakuonekana kwenye ushahidi wote wa upande wa mashtaka.
“Kutokana na hayo nashawishika na ninaamini kuwa upande wa mashtaka pasipokuacha shaka waliifungua kesi hii kwa hisia na mshtakiwa Kibanda na Makunga hawahusiki katika kuchapa wala kuhariri na kwa upande wa Mwigamba hakuandika makala kwa nia ovu,” alisema na kuongeza kuwa anawaachia huru washtakiwa wote.
Makunga
Akizungumza baada ya hukumu hiyo, Makunga alisema miaka miwili ya kesi hiyo ilikuwa ya usumbufu kwake kwa kukosa uhuru binafsi katika shughuli zake za uandishi wa habari ikiwamo zuio la kutoka nje ya Dar es Salaam bila ruhusa ya Mahakama huku hati yake ya kusafiria ikishikiliwa.
Alisema akiwa mwandishi analazimika kwenda sehemu mbalimbali ikiwamo nje ya nchi lakini yote hayo yalikuwa yakishindikana kutokana na kukosa uhuru binafsi.
Alimshukuru Mungu na Mahakama kwa kutenda haki na kuwaachia huru huku akikumbuka tukio la Agosti 2013, aliponyimwa ruhusa ya kusafiri kwenda Kenya kuhudhuria mahafali ya binti yake.
Alisema hukumu hiyo imempa nguvu ya kufanya kazi kwa bidii na kukabiliana na changamoto mbalimbali.
Kibanda
Kwa upande wake, Kibanda alisema haki ni lazima ishinde hata kama kuna nguvu za kiutawala. Alisema hilo limedhihirika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Alisema vyombo vya habari vimekuwa vikifanya kazi zake hususan kuandika habari kwa shaka na kwamba sasa uhuru wa habari umethibitika na wanahabari wanapaswa kusonga mbele.
“Mahakama imeweka alama ya kipekee, siyo Tanzania tu, bali kimataifa, vyombo vya habari bado vina alama ya kushinda,” alisema Kibanda.
Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Tido Mhando aliwataka waandishi wa habari kuzingatia misingi ya sheria na maadili ya uandishi wa habari. Alisema kilichoandikwa kwenye makala hayo kilikuwa kinaelimisha jamii.
Mhariri Mtendaji Mkuu wa MCL, Bakari Machumu alisema matukio yaliyotokea hivi karibuni yaliwatia hofu waandishi wa habari kwa kuingiliwa uhuru wao na kwamba hukumu hiyo imetoa nuru na kuwatia moyo kusonga mbele kujenga nchi.
Wakili Nyaronyo Kicheere ambaye pia alikuwa akimtetea Makunga alisema hukumu ya kesi hiyo ni ushindi kwa waandishi wa habari.
Kicheere alisema makala ya Mwigamba yalikuwa na lengo la kutoa elimu kwa vyombo vya dola kwa jinsi vinavyopaswa kuwajibika kwa wananchi.
“Nadhani hukumu hii itatoa fursa kwa waandishi wa habari kuchambua vyombo vya dola vinavyofanya kazi,” alisema.
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa