Home » » Mwizi wa fedha ATM afungwa miaka mitatu

Mwizi wa fedha ATM afungwa miaka mitatu

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imemhukumu kifungo cha miaka mitatu jela, raia wa Bulgaria, Todor Peev Peev (38) baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa fedha katika mashine ya ATM.
Hatua hiyo ilikuja baada ya kushindwa wake kulipa faini ya Sh6 milioni.
Kwa hukumu hiyo, Peev anaweza kuepuka kifungo hicho kama atamudu kulipa faini ya Sh 6 milioni mahakamani. Hivi sasa mshtakiwa yuko gerezani akisubiri kulipa kiasi hicho cha fedha.
Todor Peev alikuwa akikabiliwa na makosa 20 ya wizi wa Sh12 milioni kupitia mashine za ATM kwenye Benki ya Posta na Benki ya Afrika (Boa).
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Waliarwande Lema, alisema mahakama imezingatia kuwa mshtakiwa ni mkosaji wa kwanza na alikiri kutenda makosa hayo.
Alisema kwa msingi huo atatumikia kifungo cha miaka mitatu jela ama kulipa faini Sh300,000 kwa kila kosa.
“Hukumu hiyo imekuja baada ya mshtakiwa kukiri kuhusika na wizi huo na upande wa mashtaka ulimsomea maelezo ya awali na kuwasilisha vielelezo,” alinena.
Kwa miezi kadhaa, mshtakiwa alikuwa akisota rumande baada ya kushindwa kukamilisha masharti ya dhamana aliyopewa na Hakimu Lema Agosti 27, mwaka 2013.
Masharti hayo ni pamoja na kuwa na wadhamini wawili.
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa