Wabunge wengi wamedaiwa kutamani kunufaisha majimbo yao fedha
zilizotokana na chenji ya rada, hivyo ni changamoto kwa wizara
zilizokabidhiwa kusimamia matumizi yake.
Madai hayo yaliwasilishwa na Katibu Mkuu wa Ofisi
ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Jumanne
Sagini kwenye ripoti ya matumizi ya chenji hiyo kwa Kamati ya Bunge ya
Hesabu za Serikali.
“Ni changamoto kubwa hasa ugawaji wa madawati,
tulikubaliana tupeleke kwenye wilaya tisa ikiwamo za Mkoa wa Dar es
Salaam, lakini tulishambuliwa na wabunge hadi tulijikunyata,” alisema
Sagini.
Alisisitiza kuwa kuna wabunge wengine walidai
kwamba, hawapo tayari kukosa madawati maeneo yao kwa sababu ndiyo
walifuata chenji hiyo.
Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya
Hesabu za Serikali, Kabwe Zitto alisema iwapo watafuata matakwa hayo
itakuwa ni vigumu kuyatekeleza kutokana na mahitaji makubwa ya madawati
yaliyopo kwenye shule nyingi zilizopo nchini.
Pia, Mbunge wa Tabora Mjini, Aden Rage kwa upande
wake alishauri Tamisemi kugawa fedha zilizopangwa kugharimia madawati
kwa halmashauri, ili kuwezesha utengenezaji wa madawati mengi kwa bei
nafuu katika maeneo ambayo mbao zinapatikana.
Katika majibu yake, Sagini alikataa ushauri huo
akieleza kwamba madawati mengi ambayo yamewahi kutengenezwa chini ya
usimamizi wa halmashauri yana kiwango kisichoridhisha.
“Fedha hizi tunatakiwa kuzitumia kwa vitu vyenye kiwango,” alisema.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment