Home »
» TASO yataka wanachama kujiandaa Nanenane
TASO yataka wanachama kujiandaa Nanenane
CHAMA
cha Wakulima Tanzania (TASO) kimewataka wakulima, wafugaji, wavuvi na
wadau mbalimbali kujiandaa kikamilifu ili kushiriki Maonesho ya Nanenane
yanayotarajia kufanyika Agosti Mosi, Kanda ya Kusini na kufikia kilele
Agosti 8, mwaka huu.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa Dar
es Salaam jana na kusainiwa na Mwenyekiti wa TASO, Engelbert Moyo,
ilisema kuwa wadau hao ndiyo walengwa wa maonesho hayo hivyo hawana budi
kujiandaa kikamilifu ili kuweza kushiriki vyema.
Alisema sherehe za
maonesho hao zinatarajia kufanyika katika Uwanja wa Maonesho ya Kilimo
wa Ngongo uliopo Mjini Lindi na kwamba kulingana na taratibu za
uendeshaji maonesho hayo yatafanyika kwa miaka mitatu mfululizo katika
Kanda ya Kusini.
"Moja ya malengo ya TASO ni kushirikiana na
Serikali katika kuendeleza Viwanja vya Maonesho ya Kilimo nchini,
kuandaa sherehe na maonesho ya kilimo na Nanenane kitaifa kwa zamu
kikanda kila baada ya miaka mitatu, hivyo mwaka huu maonesho ya kilimo
yatafanyika kitaifa kwa mara ya kwanza Kanda ya Kusini,"alisema Moyo.
Alisema
madhumuni makubwa ya maonesho ya Nanenane ni kutoa msukumo maalumu
nchini kote katika kuinua kiwango cha kilimo, ufugaji, uvuvi, ufugaji wa
nyuki na kuimarisha ushirika na pia kuhimiza hifadhi ya mazingira na
kuwatukuza wahusika hao wote kwa mchango mkubwa wanaoutoa katika
kuendeleza nchi.
"Sehemu kubwa ya sherehe hizo huwa ni maonesho ya
kilimo ambayo lengo lake kubwa ni kutoa mafunzo, elimu bora ya kilimo na
ufugaji hasa wadogo wadogo ambapo wakulima na wafugaji hupata nafasi ya
kubadilishana uzoefu katika shughuli zao za uzalishaji," alisema.
Alisema
wafanyabiashara hutoa fursa nzuri ya kutangaza na kupanua soko la
bidhaa zao hususan pembejeo na zana mbalimbali za kilimo, ufugaji, uvuvi
na mambo mengine na kwa kuzingatia Katiba ya TASO moja ya majukumu ya
kazi zake ni kukuza na kuendeleza sekta hizo ikiwemo uzalishaji wa
bidhaa za maliasili na hifadhi za mazingira. Moyo alisema moja ya mbinu
kubwa ya chama hicho ya kuchangia maendeleo ya jamii yote ya Watanzania
na kuwaandaa, kuratibu, kuendesha na kusimamia maonesho hayo na ili
kuwezesha TASO itekeleze hayo.
Chanzo;Majira
0 comments:
Post a Comment