Home » » Wasomi: Kikwete amejichanganya

Wasomi: Kikwete amejichanganya

image


WASOMI nchini wameshangazwa n a Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, kwa kupuuza ushauri wa wasaidizi wake wa ndani ya chama hicho na badala yake kuamua kuendelea kuwakumbatia mawaziri wanaodaiwa mizigo.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti baadhi ya wasomi walieleza kushangazwa na mabadiliko aliyofanya katika baraza lake la mawaziri, akikataa kufanyia kazi ushauri wa msaidizi wake, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, kuhusiana na mawaziri mizigo.
 Akizungumza na gazeti hili Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mt. Augustino Profesa Mwesiga Baregu, alisema CCM imejichanganya kutokana na matamshi yaliyowahi kutolewa na katibu mkuu (Kinana) kuhusiana na maziri wote ambao walionekana utendaji kazi wao hauridhishi.
Alisema inaonekana chama hicho hakina sauti moja hata kwenye masuala yao ya sera hakuna maelewano ndiyo maana walichokuwa wakieleza wananchi kwamba mawaziri mizigo watawajibishwa, kimeshindwa kutekelezwa na Rais Kikwete.
Profesa Baregu, alisema utekelezaji wa maamuzi au maagizo yanayotolewa ndani ya chama hicho hayafanyiwi kazi kutokana na utekelezaji kukosa dira, hivyo chama hicho hakiwezi kufikia malengo.
Profesa Baregu, alisema CCM haina malengo na kama wanayo hawajatambua uelekeo wa malengo yao, ndiyo maana wanajichanganya wenyewe.
"Ninashangaa kwani Raisi uteuzi wake si sahihi, haiwezekani katika Wizara ya Maliasili na Utalii kumpandisha aliyekuwa Naibu Waziri kuwa waziri kutokana na tuhuma zilizokuwepo ndani ya wizara hiyo," alisema.
Aliongeza kuwa kutokana na Rais kuunda tume huru ya kimahakama kwa ajili ya kuchunguza tuhuma zilizotolewa bungeni kwa ajili ya wizara hiyo, naibu huyo alikuwepo wakati wa Operesheni Tokomeza.
"Hakustahili kabisa kumpandisha daraja na hata tume iliyoundwa kuchunguza hali hiyo haiwezi kupata taarifa sahihi kutokana na tuhuma hizo kwani alitakiwa na yeye kupisha uchunguzi ili uweze kufanyika,"alisema.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ally, alisema CCM inaridhika na utawala na mwelekeo uliopo na muundo wa uchumi ulivyo badala ya kutafuta kiini cha tatizo na kutatua haraka.
Alisema kuwa wamebaki wakihangaika na mfumo wa ubepari wa chuma ulete, ndiyo unaosumbua kwani bado hawajajua kiini cha tatizo wanahangaika na dalili hivyo wanatakiwa kujirekebisha.
"CCM inatakiwa kutambua kiini cha ugonjwa kuliko kuhangaika na dalili ndiyo maana Serikali ya Kikwete inakuwa nafukuza fukuza na kuchagua watu wengine hali ambayo haitafuti kiini chake," alisema Ally.
 Kwa upande wake, Profesa Abdallah Safari , alisema anashangaa kuona mwenyekiti wa CCM anapuuza ushauri wa katibu wake kwani vyama vikubwa vinakuwa na mshikamano na kauli moja, lakini kwa CCM taswira hiyo ni tofauti.
Alisema Katibu Mkuu wa CCM anawajibika na anatembea maeneo mbalimbali kusikia maoni ya wananchi na kisha anayafikisha kwenye chama na kuyatolea maamuzi, hivyo, Rais Kikwete alitakiwa kusikiliza maoni ya wananchi na wasaidizi wake.
Pia alisema Rais inaonekana uteuzi wake haukuwa sahihi kutokana na kumteua, Mwigulu Nchemba na Juma Nkamia, kwani hao wamekuwa na lugha ambayo si nzuri kwa wananchi na wapinzani.
"Inaonekana Rais Kikwete anawapenda watu wenye kauli mbaya kwa wananchi, japokuwa katiba inamruhusu kufanya uteuzi bila kushauriwa na mtu," alisema Profesa Safari.
Wakati huo huo, Mchungaji wa Kanisa la Anglikana la Msalaba Mtakatifu Bagamoyo, Kelven Ngaeje, amemtaka Katibu Mkuu wa CCM, Kinana na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya CCM NEC, Nape Nnauye, wajiuzulu kutokana na mwenyekiti wa chama hicho kukataa kusikiliza ushauri wao kuhusu kuwawajibisha mawaziri mizigo.
Akizungumza kwa simu akiwa Bagamoyo jana Mchungaji Ngaeje, alisema hakuna sababu viongozi hao kuendelea kushikilia nyadhifa hizo kwani wameshindwa kumshauri Rais Kikwete kama walivyokuwa wameahidi kuwa kwa kupitia chama chao watahakikisha wanamshauri Rais il kuwafuta kazi mawaziri waliotajwa kuwa ni mizigo.
"Mbona hatujaona ahadi zao zikitimia? Tumeshuhudia mawaziri mizigo waliokuwa wanatajwa wamerudi tena,ina maana wao wameshindwa kumshawishi Rais ili kuwaondoa mawaziri waliolalamikiwa."
Naye aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama Allience Demokratic Change (ADC) Kadawi Limbu, amemtaka Makamu Mwenyekiti Taifa wa Chama Cha Mapinduzi CCM, Philip Mangula, Kinana na Nape Nnauye kujipima wenyewe kutokana na ushauri wao kutozingatiwa

Chanzo;Majira

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa