Mkutano wa Jukwaa la Kimataifa la Uchumi (WEF) umeitaja
Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zitakazonufaika na miradi 16 barani
Afrika ambayo imepewa kipaumbele kutokana na kuzishirikisha sekta
binafsi katika ujenzi wa miundombinu.
Akitoa taarifa za mkutano huo kwa waandishi wa
habari jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison
Mwakyembe alisema Tanzania itanufaika kupitia Mradi wa Ukanda wa
Uchukuzi wa Kati (Central Transport Corridor) ambao unaiunganisha
Bandari ya Dar es Salaam na nchi za Rwanda, Burundi na Uganda kupitia
Bandari Kavu ya Isaka, Maziwa ya Tanganyika na Victoria.
Alisema Tanzania imefanikiwa kupata nafasi hiyo
baada ya kufanikiwa kuingia katika miradi 16 bora kati ya 51
iliyoshindania nafasi hiyo na kwamba mipango bora ya serikali ndiyo
iliyofanikisha uteuzi huo na kwamba baadhi ya marais waliokuwapo katika
mkutano huo walionyesha kutokuridhishwa na uamuzi uliofikiwa.
“Mara nyingi Watanzania makubwa yanayofanyika
katika nchi yetu huwa hatuyachukulii kwa umaniki. Tunapenda tu kuona
mabaya, lakini kwa wenzetu hiki ni kitu kikubwa kupita kiasi, siyo
kwamba tumependelewa, mimi ninachofahamu tunasifa,” alisema Mwakyembe.
Alivitaja vigezo vikubwa viwili vilivyotumika
kuichagua Tanzania kuwa ni mikakati mizuri iliyoainishwa na serikali
kupitia Mpango wake wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ya kuendeleza ukanda
wa uchukuzi wa Kati na msimamo wa serikali katika kufuatilia mipango
yake.
Mwakyembe alifafanua kuwa, Mwenyekiti wa Mkutano
huo uliofanyika Davos, Uswiss, Waziri Mkuu wa zamani wa Uingireza,
Gordon Brown alisema miradi iliyoteuliwa itaendelezwa kwa viwango vya
kimataifa, ili iwe mifano kwa miradi mingine ya miundo mbinu barani
Afrika.
Warsha ya maandalizi ya utekelezaji wa miradi hiyo
inatarajiwa kufanyika nchini wiki ya kwanza ya Aprili, ambapo Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni
rasmi.
Katika kufanisha mradi huo, Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda anatarajiwa kuunda kamati ndogo ya kifaifa ya wajumbe wanane
watakaosimamia mradi huo.
Mei 2012, Jukwaa la Kimataifa la Uchumi kwa Bara
la Afrika lilikutana Addis Ababa, Ethiopia, ambapo lilianzisha mkakati
wa kuhusisha sekta binafsi katika ujenzi wa miundombinu katika bara hilo
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment