Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Mwesiga Baregu
amesema, Bunge maalumu lijao la Katiba linaweza kugeuka kituko iwapo
wajumbe wake wataweka mbele masilahi ya vyama vya kisiasa na kuacha
misingi ya kujenga taifa moja na lenye mshikamano.
Pia amesema, pamoja na Tume hiyo ya Mabadiliko ya
Katiba kukamilisha kazi yake lakini kwa upande mwingine hatakubali kukaa
kimya pindi atakapoona kazi nzuri iliyofanywa ya ukusanyaji maoni ya
wananchi ikidhihakiwa.
“Sitaweza kukaa kimya eti kwa sababu Tume
imemaliza kazi yake huku nikiona watu wanapindisha mambo na kukebehi
kazi nzuri ya Tume,” alisema.
Akizungumza kwenye kongamano lilipewa jina,“Katiba
moja kwa Watanzania wote-Pamoja tutafika,” Prof Baregu alisema bila
kuweka utashi wa kujenga taifa moja, Bunge lijalo linaweza kutawaliwa na
vituko.
“Iwapo wajumbe watakwenda kwenye Bunge la Katiba
huku wakiwa na ushabiki wa vyama vyao mimi naona kutakuwa na vituko
vikubwa.Tunapaswa kutambua kwamba tunakwenda kutengeneza Katiba ya Taifa
na siyo kwa kuegemea masilahi ya kundi fulani,” alisema.
Alisema itakuwa siyo jambo la busara kuona wajumbe
wakielekea kwenye Bunge hilo huku wakiwa tayari wamevalia nguo rasmi za
vyama vyao kwani kwa kufanya hivyo kunaweza kutia doa mchakato wa
kupata Katiba Mpya.
Prof Baregu aliwataka wajumbe watakaokuwa kwenye
Bunge lijalo kutumia lugha sahihi inayoeleweka kwa wananchi badala ya
kuchanganya lugha kama inavyojitokeza sasa katika vikao mbalimbali vya
Bunge.
Henzron Mwakagenda kutoka Jukwaa la Katiba alisema ufanisi wa bunge lijalo unatia mashaka.
“Sisi tulikuwa kwa kwanza kupinga suala la wabunge
kuwa sehemu ya bunge hili na tulipinga pia Rais kuteua wajumbe.
Inavyoonekana sasa Bunge hili lijalo huenda lisiwe na tija,tunakusudia
kuandaa kongamano maalumu”.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment