Home » » Kamati ya Bunge yapigwa butwaa

Kamati ya Bunge yapigwa butwaa

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala imebaini kwamba Idara ya Mahakama katika bajeti ya mwaka 2013/14 imepewa Sh5 bilioni tu kati ya Sh43 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo William Ngeleja alisema jana kwamba kiasi hicho ni kidogo hasa ikizingatiwa kuwa bado miezi mitano kumalizika kwa mwaka huu wa fedha.
Alisema kitendo hicho kinakwamisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na hivyo kurudisha nyuma jitihada za kutaka wananchi kupata haki kwa wakati.
Juzi, Rais Jakaya Kikwete akizungumza kwenye Siku ya Sheria, alitaka wadau kushirikiana katika utendaji ili kuwawezesha wananchi kupata haki zao kwa wakati.
“Kamati inaomba Serikali iongeze speed (kasi) ya kuipa idara hiyo fedha ili iweze kukabiliana na changamoto nyingi zilizopo,.Kamati inasikitishwa kuwa muda uliobaki ni mfupi mwaka huu wa fedha lakini idara hiyo imepewa asilimia 13 tu ya fedha zilizotengwa,” alisema Ngeleja.
Alisema kamati hiyo ilikutana na Jaji Mkuu wa Tanzania, Othman Chande na kubaini kwamba licha ya mipango mizuri lakini tatizo kubwa ni ukosefu wa fedha.
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa