Wakati Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi CCM ikimpitisha
Godfrey Mgimwa (32) kuwa mgombea wa chama hicho Jimbo la Kalenga, mkoani
Iringa, Kamati Kuu ya Chadema inakutana keshokutwa kuteua jina la
mgombea wake.
Mgimwa ni mtoto aliyekuwa Mbunge wa Kalenga na
Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa aliyefariki Januari Mosi mwaka huu,
Afrika Kusini alikokuwa akipata matibabu.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na
Uenezi, Nape Nauye alisema jana kuwa jina hilo lilipitishwa kwenye kikao
cha Kamati Kuu kilichofanyika Ikulu chini ya Mwenyekiti wake, Jakaya
Kikwete.
“Kwa hiyo tunatangaza rasmi kwamba Godrey Mgimwa ndiye mgombea wa chama chetu Jimbo la Kalenga,” alisema Nape.
Kabla Kamati Kuu haijampitisha, Mgimwa wiki
iliyopita alishinda kura za maoni kwa kupata 342, huku mshindi wa pili
Jackson Kiswaga akipata kura 170, watatu ni Hafsa Mtasiwa aliyeambulia
kura 42.
Tayari Tume ya Uchaguzi imepanga Machi 16, mwaka huu kuwa siku ya uchaguzi Jimbo la Kalenga.
huku kampeni zikifanyika kuanzia Februari 19 hadi Machi 15.
Akifafanua, Nape alisema wana CCM wana imani na mgombea huyo kuwa atashinda kwa kishindo na kulichukua jimbo hilo.
Naye Ofisa habari wa Chadema, Tumaini Makene,
alisema mbali na CC kufanya uteuzi, pia itapokea ya uchaguzi wa madiwani
uliofanyika mwishoni mwa wiki.
Makene alisema pia kuwa Kanda mbalimbali
kulikofanyika uchaguzi huo, zilipewa jukumu moja la kuhakikisha mambo
yanakwenda vema, lakini kutokana na matokeo yaliyopatikana, kila Kanda
inatakiwa kuandika ripoti ya uchaguzi huo kabla ya CC kutoa kauli rasmi
ya kufanyika uchaguzi huo.
Nape ajibu hoja
Akijibu shutuma kwamba, jimbo hilo linarithishwa
kifamilia, Nape alisema chama hicho hakiwezi kumnyima mwanachama yeyote
haki ya kuwania kwa sababu tu wazazi wake waliwahi kuwa viongozi.
“CCM haiwezi kumzuia Godfey kuwania eti kwa sababu ni mtoto wa
marehemu Dk Mgimwa, yeye ana haki ya kuwania kama watu wengine
tunachoangalia ni uwezo wake na hilo limeonyeshwa baada ya wananchi wa
Kalenga kumpa ushindi wa kishindo,” alisema.
Alivionya vyama vya upinzani kwamba muda wa
kampeni ukifika kufanya mikutano ya kistaarabu kwa sababu chama hicho
hakitavumilia vurugu.
Aliwapiga kijembe Chadema kuwa wanatakiwa kuandaa
Chopa nyingi zaidi ili ziweze kuwazungusha katika kata 13 ilizopo kwenye
Jimbo hilo ili wajaribu bahati yao.
Naye Mgimwa akizungumza, aliishukuru Kamati Kuu kwa kumpitisha kuwa mgombea ubunge katika jimbo hilo.
“Natoa shukurani zangu za dhati kwa Kamati Kuu
kunipitisha kugombea ubunge, sitawaangusha,” alisema Mgimwa ambaye
anafanya kazi katika Benki ya Stanbic.
Kamati Kuu jana jioni iliendelea na kikao chake
ikiwa ni maandalizi ya Kikao cha Kamati ya Maadili kitakachokaa kesho
mjini Dodoma.
Kikao hicho kinatarajia kuwahoji baadhi ya vigogo
wa chama hicho waliokiuka maadili ikiwemo kutangaza kugombea urais
kinyume na taratibu za chama hicho
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment