Home » » Chadema yajivunia kutoa ushindani

Chadema yajivunia kutoa ushindani

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema licha ya kushinda kata tatu kati ya 27 kwenye uchaguzi mdogo wa madiwani nchini, kimetoa upinzani wa kweli kwa kusimamisha wagombea kata ambazo hakikuwa na nguvu na kupata kura nyingi.
Kilisema wanaolinganisha matokeo hayo ya udiwani na mikutano ya chama hicho ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) na Operesheni Pamoja Daima iliyofanyika hivi karibuni, wanatakiwa kuangalia kura ambazo wagombea wa chama hicho wamepata.
Katika uchaguzi huo wa madiwani uliofanyika Jumapili iliyopita, CCM kimeshinda kata 23, NCCR-Mageuzi kata moja na Chadema kata tatu ambazo ni Kiborloni, Sombetini na Njombe Mjini.
Taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene inasema watu wanalinganisha ushindi wa kata tatu waliopata na matumizi ya helikopta tatu zilizotumika Operesheni Pamoja Daima.
“Wanaosema hayo wamepotoka na hizo ni propaganda nyepesi,” inasema sehemu ya taarifa.
Alisema lengo la mikutano na Vuguvugu la Mabadiliko ilikuwa ni kuzungumzia mchakato wa Katiba Mpya, uboreshaji daftari la wapigakura, kuzungumzia rasilimali za nchi na ugumu wa maisha unaosababishwa na sera mbovu za CCM.
“Operesheni Pamoja Daima imeibua mambo mengi; Katiba Mpya, rasilimali za nchi na ugumu wa maisha unaowakabili wananchi na suala la daftari la wapigakura mpaka kufikia hatua na Tume ya Uchaguzi (NEC) kutangaza kulifanyia maboresho,” inasema.
Alisema maeneo ambayo mwaka 2010 hawakusimamisha mgombea udiwani wala mbunge, wamepata kura nyingi.
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa