Home » » Dar yanawa mikono misaada kwa wanaoishi mabondeni

Dar yanawa mikono misaada kwa wanaoishi mabondeni

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik.
 
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik, amesema serikali kwa sasa haitakuwa na msaada wowote kwa wakazi waishio mabondeni endapo watakumbwa na mafuriko katika kipindi hiki cha mvua.
Aliyasema hayo jana wakati akizungumza na NIPASHE baada ya kutaka kufahamu hatua zinazochukuliwa na serikali kuhusiana na watu wanaoendelea kuishi mabondeni katika wakati huu mvua zikiendelea kumiminika.

Alisema lengo la serikali la kuwatoa wakazi wa mabondeni lilikuwa ni kwa usalama wao lakini wahusika wamekimbilia mahakamani.

Aliongeza kuwa kinachotakiwa sasa ni kumuomba Mungu kusitokee mafuriko kwa sababu hawawezi kuingilia uamuzi wa Mahakama.

“Serikali iliamua kuwatoa wakazi wa mabondeni kwa usalama wao wenyewe, lakini wakaamua kukimbilia mahakamani. Kwa hiyo hakuna msaada wowote endapo itatokea hatari ya mafuriko,” alisema na kuongeza:

“Mimi kwa sasa naomba Mungu tu mafuriko yasitokee kwa sababu yakitokea itakuwa ni hatari.”

Wakati huo huo, Wakuu wa Mikoa ya Kilimanjaro, Morogoro na Dar es Salaam ambayo imekuwa ikikumbwa na mafuriko mara kwa mara, wamewataka wananchi wanaoishi mabonde kuhama haraka kabla serikali haijaanza kuwachukulia hatua za kisheria.

Wakizungumza katika mahojiano na kipindi cha Kumepambazuka kinachorushwa na Radio One, walisema kutokana na utabiri wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuna uwezekano mkubwa wa kunyesha mvua zitakazsababisha mafuriko.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera, alisema wananchi wanaoshi maeneo hatarishi wameshapewa maelekezo kuhama haraka na wasipofanya hivyo halmashauri za wilaya za mkoa huo zitalazimika kutumia sheria ndogo ndogo kuchukua hatua.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, alisema mkoa wake kupitia kamati za ulinzi na usalama za wilaya zote zimeanza kuainisha maeneo ambayo ni hatarishi ili wananchi wahamishwe na kupelekwa maeneo yaliyotengwa.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa