Home » » Membe apongeza Kamati Kuu CCM kwa kuwatia ‘kifungoni’

Membe apongeza Kamati Kuu CCM kwa kuwatia ‘kifungoni’

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe amepongeza uamuzi wa Kamati Kuu ya CCM kwa kuwapa adhabu ya onyo kali wanachama wake sita akiwamo mwenyewe kwa kosa la kuanza kampeni za urais mwaka 2015 mapema kabla ya muda.
Waziri Membe ni miongoni mwa wanachama sita waliohojiwa na kupewa onyo kali kwa kuanza kampeni mapema. Hata hivyo, kwenye mkutano wake na waandishi wa habari jana, alikataa kuulizwa maswali.
Vigogo wengine waliopewa onyo ni Mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira.
Wengine ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja.
“Napongeza kwa hatua iliyochukuliwa na Kamati Kuu, kila chama lazima kifuate utaratibu wa kupata viongozi wake,” alisema Waziri Membe.
Alisema utaratibu wa kuwapata viongozi usipofuatwa, utaiingiza nchi kwenye vurugu na kusababisha machafuko. Alisema uamuzi huo umeonyesha kwamba CCM ina utaratibu wake wa kupata viongozi na kwamba, adhabu hiyo inaonyesha baadhi ya wanachama akiwamo yeye (Membe) walikuwa wamekiuka.
Akitoa mfano, Waziri Membe alisema Kanisa Katoliki lina utaratibu mzuri wa kumpata kiongozi wake mkuu ambaye ni Papa.
“Mataifa mengi yameiga mambo mbalimbali yanayofanywa na Kanisa Katoliki kama vile mavazi ya mapadri yameigwa na yanavaliwa na majaji, maspika na hata wanafunzi wanasherehekea kumaliza vyuo kwa kuvaa mavazi hayo,” alisema Waziri Membe.
Hata hivyo, Waziri Membe alisema hakuna taifa lolote lililoiga utaratibu wa Wakatoliki kumchagua Papa ili kupata viongozi wao.
“Mataifa mengi yameiga mavazi ya Wakatoliki, lakini hayataki kuiga jinsi wanavyomchagua kiongozi wao mkuu,” alisema.
Alisema uchaguzi wa Papa huwa ni wa haki na kwamba, hakuna mtu anayeweza kutoa rushwa ili achaguliwe.
“Pamoja na uchaguzi kuwa wa haki, lakini mataifa hayaigi utaratibu huo ili kupata viongozi wao, ndiyo maana kwenye chaguzi mara kwa mara kunakuwa na vurugu na machafuko,” alisema.
Alisema kila chama lazima kiweke utaratibu wa haki wa kupata viongozi, ili kuepusha taifa kupata rais ambaye ni fisadi.
Wiki iliyopita Kamati Ndogo ya Maadili ya CCM, iliwahoji viongozi hao wakituhumiwa kukiuka taratibu za chama hicho kwa kuanza mapema kampeni kuwania urais. Baada ya kamati hiyo kumaliza, ilipeleka taarifa kwenye Kamati ya Maadili ya CCM ililipeleka suala hilo kwa Kamati Kuu, ambayo iliwapa karipio kali na kuwafungia kutogombea uongozi wowote ndani ya chama kwa mwaka mmoja.
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa