Home » » Vigogo wawili MSD mahakamani Dar

Vigogo wawili MSD mahakamani Dar

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Wakurugenzi wawili wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD), Meneja Ubora wa Bodi Binafsi ya Maabara ya Afya na Msajili Msaidizi wake wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka saba ya matumizi mabaya ya madaraka, uhujumu uchumi na kuisababishia Serikali hasara ya Sh3.450 bilioni kwa kuingiza nchini vitendanishi feki vinavyotumika katika upimaji wa VVU.
Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai aliwataja washtakiwa wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi Namba 8/2014 ni Mkurugenzi wa Operesheni wa Kanda ya Kaskazini wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD), Sylvester Matandiko ambaye hakufika mahakamani,ambapo mshtakiwa mwingine ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bohari Kuu ya Dawa ( MSD), Sadiki Materu ambaye pia anakabiliwa na kesi nyingine ya uhujumu uchumi Namba 5 / 2014.
Katika kesi hiyo Namba 5/2014, Materu, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Industries Ltd (TPI) kinachotengeneza Dawa za Kurefusha Maisha (ARV) nchini, Ramadhani Madabida na wenzao watatu wanakabiliwa na mashtaka matatu likiwamo la kusambaza dawa bandia za ARV na kusababisha hasara ya Sh148.3 milioni.
Wengine ni Meneja Ubora wa Bodi Binafsi ya Maabara ya Afya, Zaynab Mfaume na Msajili Msaidizi wake, Joseph Nchimbi ambao wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama, matumizi mabaya ya madaraka, uhujumu uchumi na kuisababishia Serikali hasara ya Sh3.450 bilioni.
Wakili Swai alidai katika shtaka la kwanza, kuwa kati ya Januari 20 na Julai 20, 2012 washtakiwa Matandiko, Materu, Mfaume na Nchimbi wakiwa waajiriwa wa MSD na bodi binafsi ya maabara ya afya walikula njama kwa kutumia madaraka yao vibaya kinyume na sheria.
Hata hivyo, washtakiwa walikana mashtaka dhidi yao, Hakimu Hellen Liwa aliwataka washtakiwa hao kulipa nusu ya Sh3.450 bilioni ili waweze kuachiwa huru kwa dhamana, washtakiwa hao walishindwa kukamilisha masharti hayo na kupelekwa rumande hadi Machi 6, 2014 watakaposomewa maelezo ya awali (PH).
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa