Home » » Ofisi ya Takwimu yawatupia lawama viongozi nchini

Ofisi ya Takwimu yawatupia lawama viongozi nchini

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Viongozi wengi wanafanya uamuzi wa taifa bila kuzingatia takwimu sahihi zinazotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu nchini, imeelezwa.
Akizungumza kwenye mkutano wa wahariri Dar es Salaam jana, Meneja Teknolojia na Masoko wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu nchini, Mwanaidi Mahiza alisema kuna changamoto kubwa kwa viongozi kwani wengi wamezoea kuzungumza bila kufuata takwimu sahihi.
Mahiza alisema Ofisi ya Takwimu imejitahidi kuweka ukaribu wa kutoa taarifa tangu mwaka 2001 ilipoanzisha Tovuti ya Taarifa za Jamii na Uchumi (TSED), lakini ni watu wachache wanaoitumia kupata taarifa.
Alisema tovuti hiyo inatokana na ukusanyaji taarifa za viashiria kutoka idara na taasisi mbalimbali za Serikali, kutoka vyanzo mbalimbali ikiwamo sensa ya mwaka 1967 hadi 2012, tafiti na ripoti maalumu.
Akitoa mada, Mchambuzi wa Mifumo ya Kiteknolojia kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Martin Kimaro alisema faida ya tovuti hiyo ni utunzaji na uchambuzi wa viashiria kwa makundi yenye mpangilio maalumu; afya, elimu na kilimo.
Pia, Kimaro alisema tovuti hiyo hutunza viashiria vya kupima utekelezaji wa Malengo ya Milenia (MDGs), Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) na Mkakati wa Kupambana na Kupunguza Umaskini (Mkukuta).
“Pia, huweza kupima viashiria kwa maudhui mbalimbali, vipindi maalumu kama elimu kwa wote, ulemavu, umri na uzee,”alisema Kimaro.
Hata hivyo, Mtaalamu wa Usimamizi Takwimu kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef), Edith Mbatia alisema kuna changamoto kubwa kuhusu uelewa jinsi ya kutumia takwimu kwa watu wengi hasa viongozi kwa sababu wengi wanachanganya mambo.
Ofisa Mtakwimu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Nossor Siriwa alisema kuna haja ya ofisi hiyo kuhakikisha inaongeza takwimu kwenye tovuti hiyo hasa masuala ya habari, ili kuwasaidia waandishi wa habari kwenye majukumu ya kila siku.
 Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa