Home » » Dk. Mengi: Waandishi watajeni wala rushwa hadharani

Dk. Mengi: Waandishi watajeni wala rushwa hadharani

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), Dk. Reginald Mengi (katikati) akiwa na waandishi wa habari waandamizi ambao hivi karibuni walishinda kesi ya Uchochezi, wakati wa hafla ya chakula cha mchana aliyowaandalia jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Meneja Maendeleo ya Biashara wa Mwananchi, Theophil Makunga na Mhariri Mtendaji Mkuu wa Mtanzania, Absolom Kibanda.
Mwenyekiti wa wamiliki wa vyombo vya habari nchini (MOAT), Dk. Regnald Mengi, amewaasa waandishi wa habari kuwataja hadharani watu watakaobainika kuhusika na vitendo vya rushwa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Dk. Mengi alisema tabia ya kuandika habari kwa kuyatuhumu makundi umekuwa ukiwaumiza watendaji wasafi na kuwaficha watu wenye tabia hiyo.

Dk. Mengi ambaye ni mwenyekiti Mtendaji wa IPP, alisema hayo wakati wa chakula maalum alichoandaa kwa ajili ya kuwapongeza Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda na Meneja Uendelezaji Biashara wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), Theophil Makunga, kwa kuachiwa huru katika kesi ya uchochezi iliyokuwa ikiwakabili.

Alisema katika taarifa mbalimbali zinazoandikwa juu ya rushwa, haitoi majawabu ya haraka kutokana na waandishi kugusa eneo kwa makundi, badala ya kwenda mbele kwa kufanya utafiti wa kina na kutaja mtu mmoja mmoja anayehusika kupokea au kutoa rushwa.

Alitolea mfano wa makundi yanayolalamikiwa kwa vitendo hivyo kuwa Mahakama na Polisi.

"Ndani ya jeshi la polisi kuna watendaji wasafi, hata mahakamani kuna majaji na mahakimu wanaopenda kufanya kazi kwa haki na kufuata maadili, hawa tusiwavunje moyo kwa kuwaficha watu wachache wanaowachafua, kama tukiwataja kwa majina naamini taifa litakombolewa," alisema.

Aidha aliipongeza Mahakama kwa kuwatendea haki Kibanda na Makunga, ambapo alisema kutokana na hatua hiyo imeleta matumaini mapya kwa kuwa sehemu isiyo na haki hakuna uhuru wa kweli.

KIBANDA NA MAKUNGA

Awali Kibanda ambaye ni Mhariri wa Kampuni ya magazeti ya New Habari, alimshukuru Dk. Mengi, kwa kuwa karibu kabla na baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo.

"Siku ya kwanza tulipofikishwa mahakamni, Dk. Mengi aliguswa na kutaka kuja, lakini tulipopatiwa dhamana nilimuambia asiwe na hofu," alisema Kibanda.

Alisema wakati kesi hiyo ikisikilizwa alikuwa na wakati mgumu, lakini alitiwa moyo na watu mbalimbali wakiwamo waandishi na wahariri wa habari waliokuwa wakijumuika nao kila mara.

Makunga alisema wakati kesi hiyo ilipokuwa katika hatua ya kusikilizwa hakuwa na hofu, lakini hali ilikuwa mbaya ilipofikia siku ya hukumu na kwa kuwa aliona ndiyo siku ya kwenda gerezani.

Kuachiliwa katika kesi hiyo ilifuatia baada ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, Waliarwande Lema, kutoa hukumu ya kesi ya makala iliyodaiwa kuwa ya uchochezi iliyokuwa inawakabili Makunga na Mwenyekiti wa zamani wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba kueleza ushahidi upande wa mashitaka kutojitosheleza.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa