Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
katuni ikionyesha mama akimnywesha pombe ya kienyeji mtoto wake,
imeelezwa kuwa wazazi wengi hupenda kuwapatia pombe watoto wao ili
wapate usingizi ili waweze kufanya kazi zao zingine.
Inawezekana kuwa baadhi ya wazazi mkoani Iringa, wanamuunga
mkono kwa vitendo mwanafalsafa na mwandishi maarufu wa Marekani,
Benjamin Franklin, aliyewahi kusema: “Katika mvinyo kuna hekima, ndani
ya bia mna uhuru na ndani ya maji kuna bakteria.”
Ingawa kauli ya Franklin iliishia katika maneno,
baadhi ya wazazi wakulima katika vijiji mbalimbali mkoani Iringa,
wanautekeleza usemi huo kwa vitendo kwa kuwanywesha pombe za kienyeji
watoto wao wadogo wanapokuwa shambani, ili walale usingizi ili wazazi
hao wapate nafasi ya kulima bila usumbufu.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili na kuzungumza
na baadhi ya wazazi katika maeneo hayo, umebaini kuwa utamaduni huo
umekuwapo kwa miaka mingi mkoani humo.
Baadhi ya wazazi waliozungumza na gazeti hili
wanasema kuwa ingawa bado wapo baadhi ya watu wanaoendelea na vitendo
hivyo, lakini ukweli ni kwamba tayari vijana wengi wameshapata madhara
yatokanayo na pombe hiyo ya utotoni.
Wanaofanya kitendo hicho wanasema kuwa wanapofika
shambani kwanza huwatafutia watoto wao eneo zuri la kivuli na
kuwatandikia vyema, kabla ya kuwanywesha pombe, kisha ndipo mzazi huanza
kulima.
Lameck Kihaga, mkulima katika eneo la Itagutwa,
anaeleza kuwa zamani ilikuwa kawaida kwa mzazi kumnywesha mtoto wake
kikombe kimoja au viwili vya pombe kama dawa ya usingizi.
Anasema kwamba tabia hiyo imesababisha ongezeko
kubwa la wanywaji pombe maarufu aina ya ulanzi au komoni mkoani humo
ambao bado ni vijana wadogo na wanafunzi wa shule za msingi na
sekondari.
“Naamini kabisa, hawa vijana walevi mitaani leo,
wengi wao wamelowea kutokana na tabia ya kunyweshwa pombe wakiwa bado
wadogo,” anasema Kihaga.
Kauli ya Serikali
Ofisa Maendeleo ya Jamii, Mkoa wa Iringa, Menrad
Dimoso anasema kuwa taarifa za wazazi kuwanywesha watoto wao pombe za
kienyeji wakati wa kilimo zimekuwapo muda mrefu mkoani humo, lakini siyo
tatizo kubwa.
Anasema kwamba wazazi wengi waliokuwa wakifanya
vitendo hivyo walishaacha na wanaoendeleza tabia hiyo ni wachache, hivyo
haiwezi kuwa na madhara makubwa kwa jamii.
Kadhalika ziko taarifa kuwa kuwanywesha watoto
wadogo pombe huweza kuwasababishia wapate utapiamlo na alipoulizwa
Dimoso alisema:
“Ni kweli nalijua jambo hilo, pombe inaweza kuwafanya wakapata
utapiamlo, lakini mtu wa lishe angeweza kukupatia ufafanuzi zaidi.”
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Iringa, Dk
Ezekiel Mpuya, anasema kuwa pombe hizo za kienyeji zina madhara sawa na
pombe nyingine zozote. Anataja madhara hayo kuwa ni pamoja na kuathiri
ukuaji wa mtoto kiakili na maendeleo yake ya kiafya.
“Jambo hili lilikuwa kubwa sana zamani, sijalisikia katika siku za hivi karibuni,” anasema Dk Mpuya.
Daktari Bingwa wa Watoto katika Hospitali ya
Amana, Dar es Salaam, Dk Mtagi Kibatala anasema unywaji pombe kwa watoto
wadogo una madhara makubwa kiafya ikiwa ni pamoja na kupata matatizo ya
ubongo.
Anaeleza kuwa kitendo cha mzazi kumlazimisha mtoto
wake mdogo alale usingizi kwa pombe, kinapaswa kupigwa vita kwa kuwa
kinaulazimisha ubongo wa mtoto kulala muda mrefu zaidi.
“Nimeshtushwa sana na taarifa hizo, kwa sababu
ubongo wa watoto hao hauwezi kuwa sawa, pia wanaweza kupata matatizo
kwenye ini,” anasema Dk Kibatala.
Mkazi wa Nduli mkoani Iringa, Grace Kilave
anakwenda mbali zaidi na kusema kuwa watoto wengine hunyweshwa pombe
wakiwa na umri wa kati ya miaka mitatu hadi mitano, jambo linalowafanya
kuizoea na kuiilia kila wanapoona kinywaji hicho.
“Kuna watoto wadogo wamezoea ulanzi kiasi kwamba hata hawajui tofauti ya pombe hiyo na juisi,” anasema Kilave na kuongeza;
“Ninamshukuru Mungu, mimi sikupita kwenye njia hiyo, pengine leo ningekuwa mtu tofauti kabisa.”
Kauli ya Mchungaji
Kwa upande wake, Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili
la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Mkwawa, Thadei Kihwaga,
anaitaja tabia hiyo kuwa ni mpango wa kubomoa nguvu kazi ya baadaye ya
taifa.
“Mbali na kupata utapiamlo, mtoto huyo akikua atatumia fedha zake kwa pombe na ngono zembe,” anasema Mchungaji Kihwaga.
Chanzo;mwananchi
Chanzo;mwananchi
0 comments:
Post a Comment