Home » » Kingunge: Katiba Mpya suluhisho kwa wafugaji, wahamiaji na wakulima

Kingunge: Katiba Mpya suluhisho kwa wafugaji, wahamiaji na wakulima

Mwanasiasa mkongwe,Kingunge Ngombale Mwiru.
 
Mwanasiasa mkongwe  Kingunge Ngombale Mwiru amesema katiba mpya bora ndiyo dawa itakayokomesha vita vya wafugaji , wahamaji na wakulima vinavyotokea mara kwa mara na kusababisha maafa pamoja na vifo.
Akizungumza na NIPASHE juzi, kada huyo wa CCM alisema bila kuwekwa utaratibu mzuri utakaosaidia wafugaji, wahamaji wanaohama kusaka malisho na maji kwa ajili ya mifugo yao ni vigumu mgogoro wao na wakulima kumalizika.

Kingunge alisema suala hilo  pamoja na yanayohusu wakulima wadogo , wavuvi na  mambo mengine ya msingi yakiwekwa kwenye katiba mpya yatasaidia kutoa  majibu sahihi kwa baadhi ya matatizo kama hayo.

"Ukipitia rasimu ya Katiba Mpya imejaa masuala ya uongozi na namna ya kupeana vyeo na kujinufaisha kimasilahi, mambo yenye msingi kama mgogoro wa wakulima na wafugaji yamesahauliwa," alisema Kingunge.

Alisema vita vya wafugaji,  wahamiaji na wakulima haviwezi kuisha kwa kauli za kisiasa.

"Ila ukiwekwa utaratibu mzuri utaweza kuwasaidia wafugaji kupunguza idadi kubwa ya mifugo yao, kusaidia kufanya shughuli za kiuchumi mchanganyiko na kuwezesha watoto wao kusoma na pia kuepuka mgogoro na wakulima," alisema.

Aidha mwanasiasa huyo maarufu na waziri wa zamani wa serikali za awamu zote  tangu enzi za Baba wa Taifa, alitoa ushauri wa wabunge watakaoteuliwa kushiriki mchakato wa kupatikana kwa katiba mpya kuhakikisha wanaweka mbali ushabiki wa kiitikadi, kidini na eneo walilozaliwa kwa manufaa ya taifa.

"Waweke ushabiki wa vyama, udini, ukabila na masilahi ya maeneo wanayotoka ili kuhakikisha Tanzania inapata katiba mpya bora  na siyo bora katiba mpya na kutaka ijikite katika kuendeleza na kulinda umoja wetu kitaifa, amani na utulivu kwa manufaa ya sasa na ya kizazi kijacho," alisema mkongwe huyo.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa