Home » » Baraza la Vyama vya Siasa latahadharisha kutoweka amani nchini

Baraza la Vyama vya Siasa latahadharisha kutoweka amani nchini

Peter Kuga Mziray
 
Baraza la Vyama vya Siasa,  limemweleza Rais Jakaya Kikwete kuwa kuna viashiria kadhaa  vinavyohatarisha ukosefu wa  amani nchini na kutaka hatua zichukuliwe kuepusha shari.
Mwenyekiti wa baraza hilo, Peter Mziray, alimweleza Rais Kikwete juzi wakati wa kikao cha baraza na viongozi wa vyama vyote vya siasa.

Mziray ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha APPT Maendeleo, alivitaja viashiria vinavyohatarisha uvunjifu wa amani kuwa ni tume ya uchaguzi, vyama vya siasa, tasnia ya habari, taasisi za dini na vyombo vya ulinzi na usalama.

Vingine ni kero za muungano, mgawanyo mbaya wa rasilimali hasa ardhi ambayo inachochea  migogoro ya wakulima na wafugaji, wawekezaji , masuala ya gesi, madini na mafuta na suala la vijana kumaliza elimu ya darasa la saba na kukosa kujiendeleza .

Alisema serikali inapaswa kuchukua hatua katika vyombo kama tume ya uchaguzi na vya  usalama  kuhakikisha vinafanya kazi kwa mjibu wa sheria za  nchi ili kuondoa  uonevu.

Aliongeza kuwa baraza kwa upande wake litahakikisha linatoa elimu kwa vyama vya siasa ili kutunza  amani kwani utulivu ukikosekana siasa haiwezi kufanyika kazi.

Mziray alisema katika kipindi cha mwaka jana baraza lilikutana na Spika wa Bunge, Anne Makinda, na kuzungumzia suala la amani ya nchi na hasa ustaarabu na maridhiano ndani ya Bunge.

“Kwa pamoja tunaona umuhimu wa vyama vya siasa kwamba siasa syo matusi, na baraza litahakikisha vitendo vya kutoa matusi kwenye mikutano ya kisiasa nchini vinakomeshwa,”alisema.

Kukusu mchakato wa katiba, Mziray alimpongeza Rais Kikwete kusimamia vizuri kazi hiyo ya  kupata katiba mpya na hasa kwa kuangalia zaidi maslahi ya Watanzania.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa