Mfumo wa vyama vingi vya siasa ni hali ya kuwa
na chama zaidi ya kimoja katika nchi moja. Madhumuni ya mfumo huu ni
kupanua uwanja wa demokrasia kwa wananchi na kuleta ushindani wa kisiasa
unaosaidia ukuaji wa demokrasia, uwajibikaji na kuleta maendeleo kwa
nchi husika, ukiruhusu kuwapo chama tawala au muungano wa vyama hivyo
pamoja na upinzani.
Hapa Tanzania mfumo huo ulirejeshwa mwaka 1992 na baadaye mwaka 1995 kufanyika Uchaguzi Mkuu kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Uchaguzi mwingine kwa mfumo huo umefanyika mwaka
2000, 2005 na mwaka 2010, ambapo viongozi wa vyama vya siasa wamekuwa
wakinadi sera za vyama vyao kwenye kampeni na kutoa ahadi mbalimbali.
Hata hivyo sehemu kubwa wananchi, hasa vijana
wamekuwa wakiambulia patupu kutoka kwa wagombea waliotoa ahadi kutaka
kuchaguliwa katika nafasi za uongozi ikiwamo, udiwani, ubunge hata
urais, baada ya wagombea husika kutangazwa washindi.
Wanasiasa wamekuwa wakiwatumia vijana kwa njia
mbalimbali wakilenga kutimiza malengo yao kisiasa na kupata
wanachotarajia, mwishowe kundi hilo la vijana ambalo ni nguvu kazi ya
taifa huishia kuona wengine wakifaidi mafanikio huku wao kiendelea
kubaki juani.
Kutokana na hali hiyo, uwanja wetu wa Sauti za
Vijana uliwauliza: Wanazungumziaje ushiriki wao katika siasa nchini hasa
wakati wa uchaguzi na manufaa wanayoyapata baada ya uchaguzi
kumalizika?
Vijana hao walijibu ifuatavyo:
Gabriel Majaliwa (28):
Vijana tumekuwa tukitumika vibaya, bila hata
mafanikio. Mbaya zaidi hao wanaowatumia, wamekuwa hawatekelezi yale
waliyokuwa wakiwaahidi kwenye harakati zao za kutaka kuaingia
madarakani. Nawashauri waachane na siasa.
Ramadhani Mwekwa (29):
Kwa taifa lolote linalohitaji mabadiliko, lazima
vijana wawe mstari wa mbele kwani wao ndiyo kila kitu, hivyo mimi sioni
ubaya wanapoungana na vyama wanavyovipenda wenyewe katika kudai au
kupigania mabadiliko.
Shija Tumain:
Mada hii imekuja muda mwafaka, kwani vijana wanatakiwa kujifunza
kuachana na masuala ya siasa kwani wamekuwa wakitumia muda mwingi
kuwatengenezea maisha wengine, lakini wao wanaendelea kusota na ugumu wa
maisha. Nawashauri wabadilike na kuchukua hatua zaidi.
Sophia Philimon (36):
Hata siku moja vijana hawawezi kukombolewa na
siasa, lakini wanasiasa wenyewe wanatakiwa kuacha kuwatumia vijana kwa
maslahi binafsi.
Wanawatembeza na kuwalaza njaa kwa ahadi nyingi, lakini mwishowe hakuna anayewajua tena.
Abeid Jonathan (31):
Acha vijana waendelee kutumika na wanasiasa kwani
si Chadema wala CCM walioonyesha dhamira ya kweli ya kuwasaidia. Mfano;
mwaka 2010 CCM iliwaahidi vijana ajira nyingi, lakini ajira hizo ziko
wapi?
Chadema nao wanasema wakiingia madarakani
watahakikisha wanatengeneza ajira kibao, huu wote ni uongo, hivyo
vijana wanatakiwa kujitambua
Maxmillian Nangoa (28):
Ukiangalia vikundi vya ulinzi CCM, CUF au Chadema, wengi ni vijana lakini je, wananufaika vipi?
Wengi wao wanadanganyika kwa fedha kidogo, lakini
sasa umefika wakati vijana wakatambua thamani yao na kwamba wanatumika
vibaya, mwisho wa siku wanajeruhiwa hata kupoteza maisha na hakuna wa
kuwatetea.
Godfrey Mponjole (25):
Vijana wamekuwa wakifuata mkumbo, badala ya kuona
madhara wanayoyapata katika harakati za siasa. Kubwa zaidi, wanapotezewa
muda na hakuna anayewatimizia malengo yao. Nawashauri watambue kuwa
wanasiasa sio watu wa kuwategemeza kuwatimizia ndoto zao.
Hamza Gawale (37):
Kwa siku za hivi karibuni, wazee wetu wameonekana
kupewa kisogo na vyama hivi kutokana na kutokuwa na nguvu za kushirika
katika mikutano mingi, vijana bila kutambua kuwa wanapoteza muda,
wamejikita katika siasa wakiamini CCM ikiondoka madarakani watapata
unafuu na maendeleo. Hiyo ni ndoto isiyowezi kutimizwa na chama chochote
cha siasa.
Deo Msambaki (25):
Madhara wanayopata vijana kutokana na siasa ni
makubwa, wanakamatwa na kuwekwa mahabusu, wanapigana wao kwa wao na
wengine wanapoteza maisha. Lakini ambao wanawapigania siku wakiingia
madarakani hususan bungeni unasikia wanavyoongezeana posho. Unajiuliza;
hivi wanawatetea vijana au wao na familia zao? Tuache kudanganyika
tufanye kazi.
Kashaija Johnson:
Mimi naona ni bora nguvu wanazotumia vijana katika
siasa wangezielekeza nyanja nyingine mfano; michezo, kuna uwezekano
ingewafikisha mbali vijana kwani eneo hilo hakuna bugudha kama siasa
inayotawaliwa na ura
Valentine John :Wacha vijana wenyewe watumike
kuwanufaisha wengine kwani fursa za kupata maendeleo ni nyingi. Mfano;
inawezekana wakulima wakijiunga vikundi na kuanzisha mradi wa kilimo,
hapo nina hakika utawafikisha mbali, lakini kwa kuwa wanapenda
kuandamana juani bila faida yeyote.Waendelee na siasa, lakini watambue
kuwa wanasiasa hawawezi kuwaletea mabadiliko yoyote.
Swali la wiki ijayo litakuwa:
Mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanaonekana
kuwaathiri vijana wengi hasa kimaadili. Je, nini kifanyike ili
wasiendelee kuathirika zaidi?
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment