Madalali feki wanaodai kutumiwa na Benki Kuu (BoT) wameibuka mitaani kununua noti chakavu za Tanzania na fedha za kigeni.
Baadhi ya madalali hao wanapita vituo na kwenye majumba ya watu
jijini Dar es Salaam, kutangaza kuwa wananunua noti chakavu na
kuzinunua kutoka kwa watu hasa wenye uelewa mdogo.
Wateja wanamiminika na kulipwa nusu ya thamani ya fedha walizotoa
kwa wanunuzi hao, ambao wakipokea noti ya 10,000 wanawapa Sh 5,000,
kadhalika kwa Sh. 5,000 wanapewa 2,500 hivyo kupoteza nusu ya malipo
waliyostahili.
Wateja hao walifika kwenye ofisi za NIPASHE Jumapili kutoa
malalamiko ya kupunjwa, kuibiwa fedha zao na kutaja namba ya dalali
mmoja mwenye namba 0656-105110, aliyetajwa kwa jina la Justine Mkomwa
kuwa ni miongoni mwa watu wanaonufaika na biashara hiyo maeneo tofauti
jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, walisema mara nyingi wanakutana naye Buguruni kituo cha daladala kinachotizamana na kituo cha mafuta.
Wateja hao walidai madalali wanaonunua fedha hizo wanawapunja
wanapowaletea fedha za kigeni hasa Yuro na Dola, ambazo kwa vile wengi
hawajui hulipwa chini ya thamani ya nusu ya fedha wanayodanganywa kuwa
wangepewa.
“Wananunua hata fedha za Kenya, Uganda, Oman na Rial ya Yemen,” alisema mteja ambaye hakupenda jina litajwe.
Katika mahojiano zaidi walibainisha kuwa madalali hao wa Buguruni
wananunua fedha hizo na kudai kuwa wanashirikiana na vigogo wa BoT ambao
wanazichukua na kuzipeleka kwenye akaunti zao zilizoko nje ya nchi.
Walisema vigogo hao wamewapa karatasi maalumu za kuunganisha na
kutengeneza noti zilizochakaa kabla ya kuwafikishia ili zisiendelee
kuchakaa.
Walidai kuwa awali wauza noti hao walikuwa wanajichanganya na wauza
chenji za sarafu maeneo ya mengi jijini, hasa Mwenge lakini walifukuzwa
katika kituo hicho.
Ilielezwa pia kuwa biashara hiyo imesambaa mikoani hasa Moshi na Arusha ambapo madalali hao wanauza na kununua bila kificho.
Alipohojiwa iwapo raia wanaweza kununua fedha kwani kiutaratibu
fedha chakavu hurudishwa kwenye mabenki au BoT, Naibu Waziri wa Fedha,
Mwigulu Nchemba, alisema biashara hiyo hairuhusiwi kufanywa na
madalali.
Walieleza pia noti chakavu inaporudishwa benki haipungui thamani
kama alifikisha Sh 10,000 anapewa noti mpya yenye thamani hiyo.
Alisema biashara hiyo ya madalali ni haramu na kuahidi kuviagiza vyombo vya dola kuwasaka wahusika na kusisitiza:
"Hatujawahi kuweka wakala wa kununua fedha mitaani, wala noti
chakavu hazinunuliwi bali zinarudishwa benki au BoT, hilo ni kosa nipe
muda nitaongea na vyombo vya dola ili wahusika wakamatwe," alisema.
Pamoja na maelezo hayo ya Waziri, watoa taarifa hao walisema fedha
hizo ambazo hununuliwa kwenye vituo vya daladala na mitaani ni biashara
ya ‘bingo’ inayozalisha faida ya kati ya sh. 150,000 na 300,000 kwa
wiki.
0 comments:
Post a Comment