Home » » Uda yaingiza mabasi 288 Dar

Uda yaingiza mabasi 288 Dar

Mwenyekiti wa Kampuni ya Simon Group, Robert Kisena (wa pili kushoto), akikabidhiwa funguo ya mfano ikiwa ni ishara ya kupokea mabasi 170 ya Uda kutoka kwa Makamu wa Rais wa Kampuni ya magari ya Eicher, Anurag Vohra (wa pili kulia), kwenye hafla ya makabidhiano ya mabasi hayo jijini Dar es Salaam jana. Sherehe hiyo ya makabidhiano ilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk. Charles Tizeba.
 
Shirika la Usafirishaji Dar es Salaam (UDA), jana lilizindua mabasi mapya 175 na kufanya mabasi yaliyopo kufikia 288 yatakayokuwa yanatoa huduma ya usafiri katika jiji la Dar es Salaam huku Wizara ya Uchukuzi ikiliagiza kuwa la kwanza kuingia katika mradi wa Mabasi yaendayo Kasi (Darts) kwa kuwa ina vigezo.
Mabasi hayo ni kati ya 1,000 yaliyonunuliwa na kampuni ya Simon Group ambayo inamiliki UDA ambayo hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu yatakuwa yamewasili nchini.

Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Simon Group ambayo inamiliki shirika hilo,Robert Kisena, alimweleza Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk. Charles Tizeba, kuwa shirika hilo limepanga kununua mabasi mengine 2,000 na kufikisha idadi ya mabasi 3,000 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Kisena alisema ujio wa mabasi hayo utaleta changamoto kubwa katika jiji la Dar es Salaam na kuondoa usumbufu kwa wananchi ambao wamekuwa wakigombania kupanda katika daladala kutokana na uchache wa mabasi.

“Vijana wengi wakimaliza masomo na kupata kazi wanakimbilia kuwaza kununua magari japo ajira hakuna, kwa hiyo tunataka kujenga utamaduni watu wayatumie mabasi yetu kwa shughuli mbalimbali  ili wasiwe na haja ya kununua magari,” alisema.

Kisena alisema mpango wa muda mrefu ni kwamba ifikapo Juni mwaka huu UDA itaanza kutoa huduma ya usafiri katika mikoa ya Mwanza na Mbeya na pia yatanunuliwa mabasi yatakayotoa huduma ya usafiri kati ya Dar es Salaam kwenda mikoa mingine.

Dk. Tizeba, alisema UDA iwe ya kwanza kuingia katika mradi wa mabasi yaendayo kasi ambao ujenzi wa barabara zake unaendelea vizuri katika jiji la Dar es Salaam kwa kununua mabasi makubwa yatakayokuwa na uwezo wa kuchukua abiria wengi.

Alisema kumekuwa na tatizo mashirika na makampuni yanapobinafsishwa kwa watu binafsi wanayaendesha kwa muda mfupi na baada ya kubadili malengo ya awali na kwamba serikali itakuwa inawachukulia hatua wanaofanya hivyo.

Dk. Tizeba alisema serikali inapata hasara kubwa kwa siku kutokana na tatizo la foleni linalojitokeza katika jiji la Dar es Salaam na ndiyo maana inafanya kila inavyowezekana jiji hili linakuwa na huduma za usafiri za kila aina.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa