Mwenyekiti Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala,
William Ngeleja, amewataka wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba,
wasijikite katika kujadili suala la muundo wa Serikali ya Jamhuri ya
Muungano tu, bali waangalie pia masuala mengine yanayogusa masilahi ya
nchi.
Bunge Maalumu la Katiba linatarajia kuanza vikao vyake Februari 18 mwaka huu, mjini Dodoma na linatazamiwa kukaa kwa siku 70.
Ngeleja, ambaye pia ni Mbunge wa Sengerema (CCM), alisema jana kuwa wajumbe wanapaswa kuangalia masilahi ya wananchi.
Alisema Tanzania inaundwa na wakulima,
wafanyakazi, wavuvi na wafugaji na kwamba itakuwa busara kama Katiba
Mpya, itakidhi mahitaji ya makundi haya.
“Nchi yetu ina makundi mengi, sasa itakuwa vizuri
kama Katiba Mpya itazingatia watu wote. Ila inasikitisha kuona watu
wamejikita zaidi katika suala la muundo wa Serikali ya Muungano na
kusahau mambo mengine,” aliongeza Ngeleja.
Hata hivyo, alikiri kuwa suala la muundo wa
Serikali ya Muungano ni la muhimu lakini alisema haina maana kuwa
masuala mengine yaachwe.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilitoa Rasimu ya pili ya Katiba inayopendekeza muundo wa Muungano wa Serikali tatu.
Ngeleja pia aliwataka wajumbe watakaojadili katiba
kwenye Bunge la Katiba kuhakikisha kuwa Katiba Mpya inaangalia namna
rasilimali za taifa zinavyoweza kumsaidia mwananchi wa kawaida.
“Nchi yetu imejaaliwa kuwa na rasilimali nyingi
lakini tatizo kubwa ni kuwa zimeshindwa kumnufaisha mwananchi wa
kawaida,” alisema Ngeleja, ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Nishati na
Madini.
Alitaja rasilimali kama gesi, madini na mbuga za
wanyama kuwa ni mifano ya rasimali za taifa ambazo hata hivyo,
haziwanufaishi wananchi wa kawaida.
Hali kadhalika alisema litakuwa jambo zuri ikiwa
katiba ijayo itaainisha namna viongozi watakavyosimamia rasilimali za
nchi na kuhakikisha kuwa zinamnufaisha kila mmoja.
Alisema itakuwa jambo zuri zaidi ikiwa Katiba
Mpya itajikita zaidi katika kuweka msisitizo kwa Serikali kufanya kazi
kwa uwazi zaidi na kusimamia masilahi ya watu.
Ngeleja, ambaye pamoja na kupongeza uteuzi uliofanywa na Rais
Kikwete wa wajumbe 201 wa Bunge Maalumu la Katiba, pia aliwasihi wajumbe
kuweka pembeni itikadi zao na kuweka mbele masilahi ya wananchi.
Alishauri wajumbe hao kuhakikisha kuwa wanaendesha mijadala kwa utulivu, hekima na busara.
“Hatutarajii kuwepo kwa jazba wakati wa mijadala
ya katiba. Wajumbe wanapaswa kuhakikisha kuwa wanajenga hoja zenye nguvu
badala ya kulazimisha mambo yao,” alisisitiza Ngeleja.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment