Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa
Tanzania (TMA), Dk Agness Kijazi amesema licha ya mamlaka hiyo kutoa
taarifa za hali ya hewa, watumiaji wamekuwa hawazingatii hali
inayosababisha kuendelea kutokea kwa majanga.
Dk Kijazi alisema zipo sababu mbalimbali
zinazochangia kutozingatiwa kwa taarifa hizo, ikiwamo namna
zinavyotolewa huku watu wengine wakifikiri haziwahusu.
Kutokana na changamoto hiyo, TMA kwa kushirikiana
na Serikali ya Norway imekuja na mpango wa utoaji taarifa za hali ya
hewa kulingana na mahitaji ya watumiaji.
Katika mpango huo, Norway imetoa dola 10 milioni
za Marekani kwa Tanzania na Malawi, ambazo zitatumika kuhakikisha utoaji
taarifa za hali ya hewa unafanyika kwa ufanisi ili kuepukana na
majanga.
“Huwa tunatoa taarifa lakini watumiaji wanashindwa
kuzifutilia, huenda ni kutokana na jinsi ambavyo zinatolewa matokeo
yake tunakumbana na changamoto mbalimbali za mabadiliko ya hali ya hewa
na tabianchi,” alisema Dk Kijazi na kuongeza:
“Hivyo Shirika la Hali ya Hewa Duniani, limekuja
na mpango huu kuhakikisha tunatoa taarifa sahihi kwa wakati mwafaka
kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.”
Alisema kupitia mpango huo, taarifa za mamlaka
hiyo zitasaidia nchi kuepukana na majanga mbalimbali yakiwamo ukame,
njaa na kuhakikisha kunakuwapo upatikanaji chakula salama.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Usafirishaji na
Miundombinu, Edwin Mujwahuzi alishukuru Serikali ya Norway kwa kuleta
mpango huo ambao utasaidia kwa kiwango kikubwa kuboresha huduma za hali
ya hewa nchini.
Mujwahuzi alisema mamlaka hiyo ina changamoto mbalimbali, hivyo kujitokeza wafadhili wa aina hiyo kutasaidia kukabiliana nazo.
Alisema hivi sasa dunia ina mabadiliko makubwa ya
teknolojia na kwamba, bado Tanzania haijapata vifaa vya kisasa
kukabiliana na changamoto hizo.
Mujwahuzi alisema malalamiko ambayo yamekuwa
yakielekezwa kwa mamlaka hiyo na wananchi, inatokana na kutokuwa na
uelewa jinsi inavyokumbana na changamoto kwenye utendaji wake.
Aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa kufuatilia taarifa zinazotolewa, ili kuepuka majanga.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment