Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MCHUNGAJI
wa Kituo cha Nyumba ya Maombi, kilichopo Tabata Segerea, Dar es Salaam,
Patrick Emmanuel amewataka wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba
kutanguliza hofu ya Mungu katika kipindi chote cha kujadili Rasimu ya
Katiba.
Alisema kama wajumbe watakosa hofu ya Mungu, Watanzania
wasitegemee kupata Katiba bora ambayo wataitumia kwa miaka 50 ijayo
badala yake kutakuwa na malumbano yasiyo na tija ndani ya Bunge hilo.
Mchungaji
Emmanuel aliyasema hayo mwishoni mwa wiki katika Kongamano Maalumu
lililoandaliwa na kanisa hilo ili kuombea amani itawale katika Bunge
hilo na Uchaguzi Mkuu ambao utafanyika mwaka ujao.
"Nimepata maono
ya kuombea amani ya kitaifa ndani ya nchi yetu hasa ukizingatia kuwa,
tuna mchakato mkubwa wa kupata Katiba Mpya na Uchaguzi Mkuu ujao, hivyo
lazima tuwe na hofu ya Mungu katika kipindi hiki," alisema.
Aliwataka
wajumbe wote waliopata fursa ya kuingia katika Bunge hilo, wasitafute
umaarufu wa kuongea, bali wafanye kazi iliyowapeleka ili mwisho wa siku
Taifa na wananchi wake wapate tumaini jipya kupitia katiba hiyo.
Alisema
kama wajumbe wataacha kufanya kile wanachokihitaji Watanzania, Mungu
atawaadhibu kwa sababu wananchi watakuwa na manung'uniko hivyo wao
watapa adhabu.
"Hatutaki kuona damu ikimwagika katika Taifa hili
kutokana na watu wachache ambao wametofautiana kwa sababu ya itikadi ya
vyama au siasa ndio maana watumishi wa Mungu wanafanya kazi ya kuliombea
Taifa usiku na mchana," alisisitiza.
Kwa upande wake, Diwani wa
Kata ya Segerea, Azuri Mwambagi alisema umefika wakati wa viongozi wa
dini kusimama kwa dhati kuliombea Taifa ambalo lina rasilimali za
kutosha lakini zinatafunwa na watu wachache.
Alisema vijana wengi
wamepoteza matumaini hasa wanapoona viongozi wachache wanatumia
rasilimali za nchi kujinufaisha; hivyo ipo hatari ya kuvunjika amani
iliyopo.
Kongamano hilo pia lilishirikisha watumishi mbalimbali kutoka nchi za Zambia na Namibia.
Chanzo;majira
0 comments:
Post a Comment