KATIBU
Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Dar es Salaam, Abdilah
Mihewa, amewataka wanachama wa chama hicho, Kata ya Msasani, kuacha woga
wa kuwakabili wapinzani katika kipindi cha Uchaguzi wa Serikali za
Mitaa baadaye mwaka huu.
Mihewa aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na Wenyeviti, Wajumbe wa Mashina wa kata hiyo.
Alisema
viongozi wengi wa CCM ngazi ya chini ni waoga hasa wanapoulizwa na
wapinzani chama chao kimeleta maendeleo gani kwa wananchi lakini
wanashindwa kujibu wakati kazi iliyofanywa na CCM inaonekana kwa macho.
"Waelezeni
wananchi mambo makubwa yaliyofanywa na chama tawala kupitia ilani yake
ya mwaka 2010, CCM imejenga barabara za mitaa, imesogeza huduma za maji
kwa wananchi hata kujenga shule za msingi na sekondari hivyo msikae
kimya.
"Upinzani hawana la kujivunia, kipindi hiki cha mchakato wa
kupata Katiba Mpya, tuwe ngangari kwa kutoa maoni ya Serikali mbili ili
kulinda Muungano wetu uliodumu miaka mingi," alisema.
Mihewa ambaye
alikuwa mgeni rasmi katika mkutano ulioandaliwa na Diwani wa Viti
Maalumu, Wilaya ya Kinondoni, Tatu Malyaga, pia alikabidhi vifaa vya
michezo na vitendeakazi katika mashina ambavyo ni pamoja na bendera,
kadi, jezi za mipira vikiwa na thamani ya sh. milioni 5.2.
Aliwataka
wana CCM wa Msasani kuwa na umoja katika kipindi chote cha kuelekea
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu ambapo makundi
yaliyokuwepo mwaka 2009, 2010 yavunjwe ili wapate ushindi katika kata
zote.
"Anayetaka kuendeleza makundi ndani ya chama aondoke kabisa
kabla kipindi cha uchaguzi kukijafika, si jambo jema kwa kada wa CCM
anayetaka uongozi atoe zawadi kwa wanachama na kama itabainika amefanya
hivyo, ataadhibiwa," alisema.
Alimpongeza Malyaga kwa kuonesha moyo
wa dhati wa kuwasaidia vijana na kutoa vitendea kazi kwani ni watu
wachache wenye moyo wa kujitolea kama alivyofanya diwani huyo.
Chanzo;Majira
0 comments:
Post a Comment