Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
“Hawa wa mwaka juzi (2012) D ilikuwa ni kuanzia alama 35 mpaka 39 na
mwaka 2013 ikaanzia 30 mpaka 39, kwa hiyo yawezekana kabisa kuwa matokeo
haya ni sawa na yale ya mwaka jana au ni mabaya zaidi.”
Rakesh Rajani
Licha ya Baraza la Mitihani kueleza kuwa ufaulu katika matokeo
ya Kidato cha Nne Mwaka 2013 umeongezeka kwa asilimia 15.17, baadhi ya
wadau wa elimu wamesema yawezekana matokeo hayo ama yakawa sawa na yale
ya mwaka 2012 au mabaya zaidi.
Wanafunzi waliopata daraja sifuri mwaka 2012
walikuwa ni 210,846 sawa na asilimia 56.92 ya watahiniwa 458,139,
wakati mwaka 2013, waliopata daraja hilo ni 151,187 sawa na asilimia
42.91 ya watahiniwa 404,083. Waliopata daraja la kwanza mpaka la nne
mwaka 2012 walikuwa ni 124,260 sawa na asilimia 33.54 huku mwaka 2013
waliopata daraja hilo wakiwa 126,828 sawa na asilimia 36.
Waliopata daraja la kwanza mpaka la tatu mwaka
2012 walikuwa ni watahiniwa 35,349 sawa na asilimia 9.55 huku wale wa
mwaka 2013 wakiwa 74,324 sawa na asilimia 21.09.
Mkurugenzi wa Twaweza, Rakesh Rajani alilieleza
Mwananchi jana kuwa, ni vigumu kuyafananisha matokeo ya mwaka 2013 na
yale ya mwaka 2012 kutokana na kubadilika kwa mfumo wa kuyapanga.
“Ni vigumu kuyalinganisha haya matokeo, ni sawa na
kumfananisha golikipa aliyedaka mpira wakati goli likiwa na upana wa
mita tano na mwingine aliyedaka wakati goli likiwa na mita sita.
Naye Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, Profesa Herme Mosha alisema ingawa matokeo yanaonekana kupanda,
lazima uwekezaji zaidi uwekwe kwenye sekta ya elimu.
“Matokeo bado ni mabaya ukilinganisha na hali
halisi, shule nyingi za umma zimefanya vibaya kutokana na kutokuwapo na
uwekezaji wa kutosha, lazima tuwekeze kwenye elimu,” alisema Profesa
Mosha.
Awali alama za ufaulu zilizotangazwa na Katibu
Mkuu wa Wizara ya Elimu Profesa Sifuni Mchome, ni A:75-100, B+:60-74,
B:50-59, C:40-49, D:30-39, E:20-29 na F:=0-19.
Kwa mfumo huu, alama ya ufaulu ilikuwa iwe E na CA
zilitakiwa kuchangia asilimia 40. Hata hivyo mfumo huo haukutumika kama
ilivyotangazwa na badala yake alama ya ufaulu imekuwa D na CA
zimechangia 30, jambo ambalo bado halijawafurahisha wadau.
Necta yafafanua
Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la
Tanzania (Necta), Dk Charles Msonde amefafanua juu ya mfumo uliotumika
kupanga mwaka 2013 huku akisema hata mtoto wa kidato cha pili angeweza
kufaulu mtihani huo.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi,
Dk Msonde alisema alama ya ufaulu kwenye matokeo hayo ilikuwa ni D,
lakini ili mwanafunzi awekwe kwenye fungu la waliofaulu ni lazima apate
angalau C moja au D mbili kwenye masomo yake yote.
“Kuna watu wanasema, inakuwaje mimi mtoto wangu amepata pointi
42 lakini inaonekana kapata daraja la sifuri na wapo waliopata pointi 46
lakini wapo kwenye daraja la nne.
“Mtu ukipata E zote ambazo ndiyo msingi wa kupata
pointi, utaonekana una pointi 42, na mwingne akapata F sita na C moja
anaonekana amefaulu licha ya yeye kuwa na point 46,” alisema.
Akifafanua juu ya alama zilizotumika kwenye
mtihani huo, alisema A: 1, B+:2, B:3, C:4, D:5, E:6 na F:7. na kwamba
A:75-100, B+:60-74,B:50-59,C:40-49,D:30-39,E:20-29 na F:0-19.
“Kwa upande wa pointi, Daraja la Kwanza awali
ilikuwa ni kuanzia pointi 7- 17, na halikubadilika, daraja la pili
ilikuwa ni 18-21 sasa ni 18-24, daraja la tatu zamani 22-25 sasa hivi
25-31, daraja la nne zamani ilikuwa 26-32 sasa ni 32-46 na sifuri zamani
ilikuwa ni 33-35 sasa ni 47-49,” alisema.
Akizungumzia ubora wa matokeo hayo, alisema kuwa 2013 watahiniwa wamejitahidi ukilinganisha na wale wa 2012.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment