Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amesema Tanzania imeshuka kwa nafasi
tisa katika orodha ya nchi zinazofanya biashara duniani zilizopo kwenye
viwango vya Benki ya Dunia (WB) na kwa sasa inashika nafasi ya 145 kati
ya nchi 189.
Akizungumza juzi katika Uzinduzi wa Ripoti ya
Mapitio ya Sera ya Uwekezaji nchini, Waziri Pinda alisema Tanzania
inaweza kunufaika katika uwekezaji kama itatekeleza kikamilifu mapitio
ya Mfumo wa Uwekezaji yaliyowasilishwa na Taasisi ya Ushirikiano wa
Kiuchumi na Maendeleo (OECD) katika Ripoti ya Mapitio ya Sera ya
Uwekezaji.
“Ripoti inaonyesha Tanzania imeshuka nafasi tisa
na inaeleza maeneo yenye changamoto na kuchangia kushuka kwa ufanyaji wa
biashara ambao ni pamoja na upatikanaji wa mikopo, rushwa, vibali,
biashara mipakani, ulipaji kodi na usajiliwa ardhi na mali,” alisema
Pinda.
Katika hotuba yake Pinda aliwataka watendaji wa
Serikali kupitia kwa kina mapitio ya ripoti hiyo na kutumia mapendekezo
yake ili kufikia malengo ya uwekezaji yaliyowekwa katika Mpango wa
Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Alifafanua kuwa ili kukabiliana na changamoto
hizo, Serikali imeanzisha kituo katika Bandari ya Dar es Salaam ili
kuondoa vikwazo katika barabara kubwa na kurahisisha ulipaji kodi.
Alisema malengo ya mapitio ya ripoti hiyo ni
kuboresha hali ya uwekezaji na biashara nchini ambayo matokeo yake
yatasaidia kuongeza wawekezaji.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment