Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN)
umedhamiria kufanya uwekezaji unaofikia kiasi cha Dola za Marekani
bilioni moja sawa na Shkatika kipindi cha miaka michache ijayo.
Uwekezaji huo, ambao sehemu yake tayari umeshaanza, utaelekezwa katika sekta za afya na elimu.
Taarifa iliyotolewa mwishoni mwa wiki, inasema
kuwa AKDN imepanga kuwekeza kiasi cha Dola 800 milioni kwa ajili ya
upanuzi wa Chuo Kikuu cha Aga Khan kilichopo Arusha; Dola 80 milioni kwa
ajili ya awamu ya pili ya upanuzi wa Hospitali ya Aga Khan iliyopo Dar
es Salaam na kiasi kingine cha Dola 30 milioni zitatumika kuimarisha Aga
Khan Academy iliyopo Dar es Salaam.
Uwekezaji huu ni pamoja na uwekezaji mwingine
katika maeneo mbalimbali, ikiwemo kuwawezesha wakulima katika Mikoa ya
Kusini mwa Tanzania na wameweza kuongeza uzalishaji kwa takriban mara
tatu zaidi baada ya kuanza kupokea msaada kutoka AKDN.
Taarifa kuhusiana na uwekezaji huo zinakuja wakati
taasisi hiyo imeandaa maonyesho makubwa yanayofunguliwa jijini Dar es
Salaam Jumamosi ijayo.
Pamoja na wageni wengine, maonyesho hayo
yatatembelewa kwa nyakati tofauti na Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib
Bilal, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi.
Maonyesho hayo yenye kaulimbiu isemayo ‘Rays of
Light; Glimpses into the Ismaili Imamati’ yanalenga kuonyesha jitihada
za Mtukufu Karim Aga Khan kuisaidia jamii katika kipindi cha miaka 50
iliyopita.
Maonyesho kama hayo tayari yameshafanyika Paris,
Dubai, Lisbon, Uganda, Canada na Marekani katika pia kusheherekea miaka
1,400 ya historia ya madhehebu hayo duniani.
“Kwa kuwa Tanzania ni moja ya nchi zenye uwekezaji
mkubwa ikiwamo Chuo Kikuu cha Aga Khan kule Arusha, Aga Khan Academy
jijini Dar es Salaam na awamu ya pili ya upanuzi wa Hospitali ya Aga
Khan, maonyesho haya yatasaidia kutoa mwanga wa nini Mtukufu Aga Khan
amekuwa akifanya kama Kiongozi Mkuu wa Shia Imami Ismaili,” alisema
Jehangir Bhaloo, Rais wa Kamati ya Aga Khan nchini Tanzania.
Kituo cha Matibabu ya Saratani kilichofunguliwa
katika Hospitali ya Aga Khan wiki iliyopita ni moja ya uwekezaji mkubwa
unaofanywa na AKDN nchini.
Pamoja na mambo mengine, upanuzi huo utahusisha
pia vitengo vya upasuaji, magonjwa ya moyo, sayansi ya mishipa ya
fahamu, huduma muhimu na afya ya mama na mtoto.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kituo hicho,
Princess Zahra Aga Khan, alisema upanuzi huo utahusisha ujenzi katika
eneo lenye ukubwa wa meta za mraba 13,000 na ukarabati katika eneo lenye
ukubwa wa meta za mraba 6,000.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment