Home » » Tucta yamruka Mweta wa Kilimanjaro

Tucta yamruka Mweta wa Kilimanjaro

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta) limeeleza kusikitishwa na utata wa wanawake wawili wenye majina yanayofanana kuwasili katika Bunge Maalumu la Katiba mjini Dodima kwa nafasi ya ujumbe wa Bunge hilo kilisema halimfahamu Amina Mweta wa Kilimanjaro.
  Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake jana, Katibu Mkuu wa Tucta,  Nicholaus Mgaya alisema, mazingira ya  tukio hilo yamewatisha, hivyo  kulazimika kumwandikia barua Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue ili kumthibitisha mjumbe wao halali.
 “ Kwa kweli tumeshtushwa na taarifa hizo za kujitokeza mjumbe mwenye jina linalofanana na mjumbe wetu, hivyo tumelazimika kuandika barua kwa Katibu Mkuu Kiongozi na kwa Katibu wa Bunge ili kumthibitisha mjumbe wetu halali tunayemtambua ambaye ni Amina Mweta kutoka mkoani Songea,” alisema Mgaya.
 Alifafanua kwamba, mjumbe anayetambuliwa na Tucta ni Amina Mweta ambaye ndiyo jina lake lilipelekwa kwa Rais ili kufanyiwa uteuzi, likiwa pamoja na majina ya wawakilishi wa vyama vingine vya wafanyakazi.
 “ Mweta huyo tunayemtambua ana umri  miaka 43 ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa Chama cha Wafanyakazi wa Mawasiliano na Usafirishaji (COTWU) kutoka Songea, hivyo tunaamini kwamba viongozi hao watatuelewa ili mjumbe huyo aendelee kushiriki kama mwakilishi wetu halali,” alisema. Mgaya hata hivyo, alieleza kwamba tukio hilo limewashangaza kwamba baada ya mjumbe huyo mwingine kujitokeza na kudai kwamba alipigiwa simu na Ofisi ya Bunge na kupewa taarifa za kuchaguliwa.
 “Kinachoshangaza na kuonyesha kwamba kuna jambo lisilo la kawaida katika tukio hili ni kwamba namba za huyo Mweta asiye mjumbe halali zilipatikana wapi hadi wampigie simu, tunaomba vyombo husika vichunguze suala hili kwa umakini, huu ni mchezo wa hatari fedha ya Serikali tayari inadaiwa kutumika,” alisisitiza Mgaya.
 “ Jambo lingine ni  kwamba hata katika Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU) anachodai kutoka huyo Mweta wa Kilimanjaro  hawakuwa wamependekeza jina lake,  bali walipendekeza Edna Mwaigomole ambaye ni Mwenyekiti TALGWU kutoka Mbeya na Sudi Madega Katibu wa TALGWU Dar es Salaam ambao hawakubahatika kuchaguliwa na Rais,”alisema Mgaya.
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa