Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Wanawake Tanzania, Margareth Chacha
Mjumbe wa mradi wa Mwanamakuka (Mwanamakuka Award) na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Wanawake Tanzania, Margareth Chacha, aliwaambia waandishi wa habari mwishoni mwa wiki kuwa siku hiyo ni ya muhimu kwa wanawake kwa vile itawaleta pamoja na kujadili masuala mbalimbali.
“Tutakutana Siku ya Wanawake Duniani na kujadili namna bora zaidi ya kumuwezesha mwanamke kujiinua kiuchumi,” alisema.
Alisema benki yake inafadhili washindi wanawake wajasiriamali kupitia mradi huo na inafanya hivyo kwa ajili ya kumwinua mwanawake kupitia benki yao ya wanawake.
Alisema benki hiyo inataka kuona wanawake wengi wanaingia katika shughuli za kijasiriamali na pia imejipanga kutumia matawi yake nchini kupanua wigo wa zawadi ya Mwanamakuka.
Alisema mpaka sasa ni asilimia mbili tu ya wanawake wanaotumia huduma za kibenki kati ya asilimia nane ya Watanzania wote wanaotumia huduma hizo, na sasa wakati umefika kuongeza idadi ya wanawake.
“Hali hiyo ni ya kihistoria lakini kwa sasa wanawake tunashukuru hali imebadilika tunaweza kufanyakazi mbalimbali zikiwamo za biashara,”aliongeza.
Alisisitiza umuhimu wa wanawake kujiunga katika vikundi kwa ajili ya kupata mikopo kutoka katika benki yao kufanyia shughuli zao za kijasiriamali.
Naye Meneja wa mradi wa Mwanamakuka ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kituo cha Wanawake Marafiki (UWF), Maryam Shamo, alisema Siku ya Wanawake Duniani kutakuwa na maonyesho ya kazi za kijasiriamali za wanawake na michezo mbalimbali.
“Siku hiyo washindi wa mwaka huu watapatiwa zawadi zao, na pia mshindi wa jumla wa mwaka 2012 na 2013 atapatiwa zawadi kati ya washindi kumi waliokwisha pata zawadi,'' alisema.
Alifafanua kuwa katika kusherehekea ya siku hiyo, watu wengi wamealikwa wakiwamo akinamama wajasiriamali na wanasiasa wanawake.
Kwa upande wake, mjasiriamali mkazi wa Dar es Salaam na mshindi wa nyuma wa mradi huo, Tatu Ngao, alisema alishinda Shilingi milioni sita ambazo zimemwezesha kufanya biashara yake kwa ufanisi.
“Nilishinda kupitia biashara yangu ya kutengeneza keki...nimepanuka kwa kiwango cha kuridhisha hadi sasa,” alisema.
Zawadi ya Mwanamakuka ni mradi uliobuniwa na Kituo cha Wanawake Marafiki kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali wanawake kwa ufadhili wa Benki ya Wanawake Tanzania na wadau wengine.
CHANZO:
NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment