WAWEKEZAJI
wa ndani na nje ya Tanzania wamehamasishwa kuchangamkia fursa katika
maeneo maalum ya uwekezaji yaliyo katika kanda ya ziwa.
Kwa mujibu wa
taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa Dar es Salaam jana, ilimnukuu
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ukanda Maalum wa Uwekezaji (EPZA), Dkt.
Adelhelm Meru, akitoa mwito huo alipokuwa akiwasilisha mada inayohusu
fursa za uwekezaj ikatika maeneo maalum ya uwekezaji wakati wa kongamano
la uwekezaji lililomalizika hivi karibuni jijini Mwanza .
Alisema
tayari jumla ya ekari 3,500 zimeshatengwa katika maeneo ya Usagara na
Nyangamango Wilaya ya Misungwi, Mwanza pakiwa na mpango wa kuyaendeleza
kuwa mji wa biashara wenye viwanda vya kisasa.
Pia jumla ya ekari 1,000 zimeshatengwa katika Wilaya ya Kahama katika Mkoa wa Shinyanga kwa ajili hiyo .
Akifafanua
zaidi alisema jumla ya ekari 1,360 zimetengwa wilayani Bunda, Mkoa wa
Mara. Eneo hilo pia linakaribishwa kwa wawekezaji kujenga miundombinu,
viwanda na mji wa kisasa wa biashara.
"Tutaendelea kwa kushirikiana
na mamlaka za mikoa kutenga maeneo zaidi ya uwekezaji katika mikoa ya
Kagera, Simiyu na Geita," alisema.
Akielezea faida za kuwekeza
katika maeneo maalum ya uwekezaji katika kanda ya ziwa, alisema
uwekezaji katika maeneo hayo unasaidia kukuza teknolojia, kuongeza
thamani bidhaa, biashara kati ya nchi na nchi, kuongeza ajira,
kuongezeka kwa mapato ya kodi kwa mamlaka za ngazi ya chini ni miongoni
mwa faida nyingine.
Alisema mfumo huu wa uwekezaji ni maarufu sana
Asia, Mashariki ya Mbali na Mashariki ya Kati na kuwa nchi kama China,
India Malaysia, Thailand, Vietnam, Korea, na Philipines zimeimarisha
sana uchumi wake kwa kuwekeza katika maeneo maalum ya uwekezaji.
Akitoa
mfano zaidi alisema katika miaka 30 iliyopita nchi ya China imefanya
kile kinachoonekana kama 'miujiza' kutokana na maendeleo iliyojipatia
katika maendeleo ya haraka ya uchumi katika historia ya mwanadamu.
Akitumia
takwimu za Benki ya Dunia, Dkt. Meru alisema pato la ndani la nchi hiyo
limekuwa kwa zaidi ya wastani wa asilimia 9 na mwaka 2010 iliishinda
Japan na kupanda kuwa nchi ya pili kwa uchumi mkubwa duniani.
"Ingawa
wataalamu, watunga sera, wafanyabiashara mbalimbali na wasomi
wanajiuliza siri ya mafanikio hayo, kitu kimoja kilicho wazi ni kuwa
uwekezaji katika maeneo maalumu na viwanda vimekuwa kichocheo kikubwa
sana chama endeleo ya China," alisema.
Alisema mamlaka ya EPZA
imeshatenga maeneo katika mikoa 19 yenye ukubwa wa hekta 500-9,000 kila
moja nchini na kuwakaribisha wawekezaji kujenga miundombinu katika
maeneo hayo.
Alitaja maeneo ya fursa katika kanda hiyo kuwa pamoja na
kujenga viwanda kwa ajili ya kuongeza thamani mazao ya kilimo, ngozi,
madini , samaki, asali, TEHAMA na biashara.
Mamlaka hiyo inazidi
kujenga mizizi nchini. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, pamoja na
kujiwekea malengo ya kuvutia mtaji wa dola za Marekani 300 milioni kwa
mwaka jana, mamlaka hiyo iliweza kuvuka lengo na kuingiza nchini mtaji
wa jumla ya dola za Marekani milioni 498 nchini, ikiwa ni thamani ya
fedha za wawekezaji walioingia nchini kwa mwaka huo.
Pia mamlaka hiyo
ilikuwa imejiwekea lengo la kuzalisha ajira 5,200 kwa mwaka jana,
lakini hadi kufikia Desemba jumla ya ajira 10,200 zilikuwa zimezalishwa
kutokana na uwekezaji mpya uliofanywa kupitia mamlaka hiyo.
Taarifa
zinaonesha kuwa EPZA ilikuwa imejiwekea lengo la kuuza nje bidhaa zenye
thamani ya dola milioni 100 mwaka 2013 lakini lengo lilivukwa na kufikia
dola milioni 105 hadi kufikia mwishoni mwa mwaka jana.
Chanzo;Majira
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment