Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tizeba akiwaonyesha wajumbe wa
Kamati ya Bunge ya Miundombinu picha ya moja ya viatu vilivyokuwa na
dawa za kulevya vilivyokamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, jana. Viatu hivyo vilikuwa
vikisafirishwa kwenda Liberia
Wasafirishaji wa dawa za kulevya wamebuni mbinu mpya baada ya
Kikosi cha Polisi cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere
(JNIA) kukamata kilo 3.5 za heroini zikiwa zimefungwa kwenye vifurushi
zikipelekwa Monrovia, Liberia.
Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya Kikosi cha
Wanamaji cha Polisi kukamata jahazi likiwa na kilo 201 za heroini wakati
likisafiri kati ya Dar es Salaam na Zanzibar.
Mkuu wa Upelelezi wa Viwanja vya Ndege Tanzania,
Hamad Hamad alisema jana kuwa kifurushi hicho kilikamatwa Jumatatu saa
tisa alasiri, kwenye uwanja huo.
Hamad alisema mmiliki wa kifurushi hicho
kilichokuwa kinasafirishwa na Kampuni ya Kusafirisha na Kupokea Mizigo
(DHL) hajafahamika.
Kwa mujibu wa Hamad, mmiliki wa mzigo huo alikuwa ametumia jina la bandia pia maelezo ya mzigo ule yalikuwa ya uongo.
Hamad alisema dawa hizo zilikuwa zimeingizwa ndani
ya kandambili huku zikiwa na vifurushi vingine kwa ajili ya
kusafirishwa kwenda Liberia.
“Kampuni ya DHL walipewa kazi ya kusafirisha mzigo huo na kujitetea kuwa hawakuelewa kulikuwa kitu ndani,” alieleza Hamad.
Hamad alisema kuwa polisi waliutilia shaka mzigo ule wakati ukipitishwa na kuamua kuukagua, ndipo wakakuta ni heroini.
Katika hatua nyingine, Kamishna wa Kikosi cha
Kupambana na Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa alisema bado wanaendelea
kuwahoji watu 12 raia wa nchi za Iran na Pakistan waliokamatwa juzi na
kilo 201 za heroini.
Alisema pia wanaendelea kumchunguza raia wa Kenya,
Abdulrahman Salim, ambaye alikamatwa na kete 142 za dawa za kulevya
aina ya cocaine kwenye Uwanja wa JNIA.
Salim alikamatwa akitokea Brazil akiwa amepanda ndege ya Shirika la Ndege Ethiopia.
Mbinu zaidi
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tizeba ameelezea mbinu
mbalimbali zilizobuniwa na wasafirishaji wa dawa za kulevya,
zilizobainika baada ya watu saba walikamatwa katika matukio saba
tofauti.
Dk Tizeba alisema hata vitabu vimekuwa vikitumika
ambapo wahusika wamekuwa wakikata katikati ya vitabu hivyo na kuweka
kete za dawa za kulevya kabla hawajavisafirisha nje ya nchi. Hata hivyo
jambo hilo sasa wamelishtukia na udhibiti umeongezwa katika viwanja vya
ndege.
“Hivi karibuni tumekamata kitabu cha somo la
baiolojia kikisafirishwa kwenda Liberia na kilitiliwa shaka na
kilipofunguliwa kilikutwa na kilo mbili za dawa za kulevya,” alisema.
Alisema wameamua kusafarisha kwa njia hiyo baada
ya kuona mpango wa kumeza umedhibitiwa na hadi sasa wahusika wa matukio
hayo saba wamekamatwa, na mmoja bado ila huenda akatiwa mbaroni wakati
wowote.
“Saba tunao kwa mahojiano na mwingine ambaye anahusika na kitabu hicho cha baiologia anafuatiliwa,” alisema.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment