Home » » Zahanati Kinondoni zajengwa kiholela

Zahanati Kinondoni zajengwa kiholela

Tathmini ya huduma za afya katika Zahanati na Hospitali za Manispaa ya Kinondoni inaonyesha kuwa, kutokuwapo na mawasiliano miongoni mwa mamlaka za Serikali kumechangia kutokea kwa hasara ambazo zingeweza kuepukika.
Akiwasilisha ripoti ya tathmini iliyofanywa na Sikika chini ya Mradi wa ufuatiliaji na uwajibikaji kwa jamii (SAM), Mwenyekiti wa mradi huo, Alex Mwidima alisema majengo mengi ya zahanati za manispaa hiyo yalijengwa bila kupimwa hivyo kutakiwa kubomolewa.
Alitoa mfano wa zahanati ya Wazo ambayo inatakiwa kuvunjwa ili kupisha bomba la Maji la Dawasco ikiwa ni matokeo ya jengo hilo kujengwa bila kupimwa.
“Pamoja na changamoto kadhaa, tumegundua hospitali na zahanati nyingi ndani ya manispaa zimejengwa bila kupimwa na matokeo yake hasara kutokana na nyingi kutakiwa kubomolewa,” alisema Mwidima
Aidha ripoti hiyo imebainisha matumizi fedha tofauti na maelekezo yaliyotolewa kwa kazi husika.
Akiwasilisha sehemu ya tamthimi hiyo, Samwel Mhando ambaye ni Mjumbe wa SAM aliitaja Hospitali ya Mwananyamala kupatiwa Sh31.8 milioni kwa mwaka 2011/2012 kwa ajili ya upanuzi wa chumba cha kuhifadhia maiti, lakini fedha hazikutumika kama ilivyokusudiwa.
Kwa mujibu wa Mhando hakuna upanuzi wowote uliofanyika katika hospitali hiyo, huku vitabu vya manispaa vikionyesha fedha hizo tayari zimeshatolewa.
Alisema fedha hizo zilitolewa ili kupanua chumba hicho ili kiweze kuchukua miili 50 badala ya 15.
Akijibu kuhusiana na hilo Mratibu wa Mipango ya Afya Manispaa ya Kinondoni, Dk Ezra Ngereza alisema hospitali ilifikia uamuzi wa kusogeza mradi wa upanuzi wa chumba hicho kwa sababu maalumu. “Kulikuwapo malalamiko ya Waislamu na Wakristo kupinga maiti kuoshwa chumba kimoja, hivyo fedha hizo zitumike kujenga vyumba viwili.” alisema.
Chanzo;Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa