Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Wakati haijafahamika nani aliyelipwa mabilioni ya shilingi yaliyokuwa kwenye akaunti ya Escrow katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kutokana na mvutano baina ya Tanesco na Kampuni ya IPTL, imebainika kuwa Bunge liliwahi kuagiza fedha hizo zisichukuliwe mpaka mitambo ya IPTL itakapokuwa chini ya Tanesco mwakani.
Hiyo imo katika taarifa ya iliyokuwa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), kwa mwaka wa
fedha ulioishia Juni 30, 2007.
Hata hivyo, Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu
alithibitisha jana kuchotwa kwa Dola za Marekani 122 Milioni (Sh195.2
bilioni) katika akaunti hiyo, lakini akakataa kutaja nani hasa
aliyelipwa.
Mkataba wa miaka 20 baina ya IPTL na Tanesco
ulisainiwa mwaka 1995 na ulitakiwa kuisha 2015 na mitambo hiyo kuwa mali
ya Tanesco.
Hata hivyo, ukiwa umebaki mwaka mmoja kumalizika,
imebainika kuwa mitambo hiyo imeuzwa kwa Kampuni ya Pan African Power,
ambayo inatarajiwa kuingia mkataba mwingine na Tanesco ili iwauzie
umeme.
Ndulu alisema fedha zilizokuwa kwenye akaunti hiyo
ni Dola za Marekani 22 milioni na Sh161 bilioni za Tanzania ambazo zote
kwa pamoja ndizo zilizofikisha jumla ya Sh195.2 bilioni.
Vyanzo vingine vilitoa takwimu mbili tofauti,
kimoja kikisema kiasi cha fedha hizo kilifikia Dola za Marekani 270
milioni na kingine Dola 250 milioni. Kuhusu nani mwenye mamlaka ya kutoa
fedha hizo, Profesa Ndulu alisema kwa mujibu wa mkataba wa kufunguliwa
kwa akaunti ya fedha hizo, ni Wizara ya Nishati na Madini pamoja na
IPTL.
“Hakuna mtu mwingine anayeweza kuidhinisha
kutolewa kwa fedha hizo zaidi ya hao, kwa hiyo hao ndiyo waliosaini
kutolewa kwa hizo fedha na taratibu zote zilifuatwa,” alisema Profesa
Ndulu.
Alipoulizwa ni nani aliyelipwa fedha hizo, Profesa
Ndulu alisema IPTL ndiyo iliyokuwa na mamlaka ya kusema ni nani alipwe
na ilifanya hivyo.
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim
Maswi alipoulizwa juu ya fedha hizo alisema: “Kwa kawaida huwa nina
majibu mafupi sana, lakini kwa kuwa mmeamua kuandika uongo, endeleeni,
siwezi kukujibu chochote wasiliana na hao IPTL wakujibu.”
Hata hivyo, haikuwa rahisi kumpata kiongozi wa IPTL kuzungumzia suala hilo kwa kuwa tayari kampuni hiyo ni mufilisi.
Msimamo wa Bunge
Ripoti ya POAC inasema Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali
(CAG) aliorodhesha matatizo ya mkataba kati ya Tanesco na IPTL na
kuangalia mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na mipango ya kununua mitambo
hiyo na kuibadilisha iwe inatumia gesi badala ya mafuta mazito.
“Mgogoro uliopo hivi sasa kati ya Tanesco na IPTL
unahusu kiwango cha malipo ya uwekezaji yaani capacity charges ambacho
IPTL walikuwa wanalipwa na Tanesco. Kwa mujibu wa mkataba huo, capacity
charge inapaswa kukokotolewa kwa kuzingatia mtaji wa asilimia 30 na
mkopo wa asilimia 22.31.
Baada ya uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa, ilikubalika kuwa mtaji uliowekezwa uwe ni Dola za Marekani 36 milioni.
Hata hivyo, baada ya uchunguzi wa Tanesco iligundulika kuwa IPTL haikuwekeza fedha hizo, bali Sh50,000,” inasema ripoti hiyo.
Ilisema kuwa, mpaka kufikia Mei 2008, Tanesco ilikuwa imeilipa IPTL Sh221 bilioni tangu ilipoanza uzalishaji umeme Januari 2002.
Kamati iliagiza: “Wanasheria wa Tanesco na
Serikali watumie ushahidi wote uliopo kuhakikisha kuwa kiwango cha fedha
kilichopo kwenye akaunti maalumu (Escrow) ndicho hichohicho kitumike
kumaliza madeni yaliyopo na vilevile kufanyia marekebisho mitambo hiyo
ili itumie gesi,” inasema taarifa hiyo.
Pendekezo hilo lilipitishwa na Bunge huku POAC
ikitoa maelekezo kwa Gavana Ndulu kuwa fedha zilizopo Escrow zisitumike
kwa namna yoyote ile bila mitambo ya IPTL kuwa ya umma na kubadilishwa
na kutumia gesi asilia.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa POAC, ambaye sasa ni
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe
alisema ameshtushwa na taarifa za kutolewa kwa fedha hizo kinyemela.
“Tunaitaka Serikali kutoa taarifa kama kweli hizo
fedha zimetolewa, kwa sasa siwezi kutoa msimamo wetu kwa kuwa hatujakaa
kama kamati, tunatarajia kuitisha kikao cha dharura Dodoma kuzungumzia
suala hili,” alisema Zitto.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment