Home » » Serikali inafaidika na migogoro ya walimu?

Serikali inafaidika na migogoro ya walimu?

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

   Kama tulivyosema hapo juu, watakaoumia ni wanafunzi na wazazi wao na si viongozi serikalini wanaotunga sera ambazo zinaonekana kuwakandamiza walimu na taaluma yao. Tunasema hivyo kutokana na Serikali kutoshughulikia kero za muda mrefu za walimu

Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kimetangaza mgogoro na Serikali kwa kushindwa kufanyia kazi madai mbalimbali ya walimu yanayofikia Sh61 bilioni, yakiwamo malimbikizo ya mishahara na likizo za walimu. Madai mengine ni Serikali kutokufanya maandalizi mazuri ya mfumo wa kutathmini utendaji wa walimu kwa lengo la kuwapandisha madaraja.
Rais wa CWT, Gratian Mukoba alisema juzi kwamba chama hicho kimefikia uamuzi huo baada ya kuona kuwa katika madai hayo matatu hakuna hata moja lililofanyiwa kazi na Serikali ambayo amesema imekuwa ikitoa ahadi za uongo. Kwa mujibu wa kiongozi huyo, Baraza la Taifa la CWT lilikutana Januari 27 hadi 29 mwaka huu na kuazimia kwamba kero hizo za walimu ziwe zimepatiwa ufumbuzi mwishoni mwa mwezi uliopita, vinginevyo chama hicho kitangaze mgogoro na Serikali.
Hizi siyo habari njema hata kidogo kwani uzoefu umetuonyesha kuwa, kila itokeapo migogoro na mikwaruzano kati ya walimu na Serikali, wanafunzi na wazazi wao ndio huwa majeruhi wa kwanza. Katika hali kama hiyo, tumeshuhudia mara nyingi Serikali ikitoa machozi ya mamba ikijifanya kuguswa pale inapolalamikiwa na wananchi kwa kusababisha walimu kususia masomo na wanafunzi kukosa walimu wa kuwafundisha.
Hivyo, mgogoro huo uliotangazwa na CWT unaashiria balaa kubwa la uwezekano wa kutokea mgomo wa walimu nchi nzima. Kama tulivyosema hapo juu, watakaoumia ni wanafunzi na wazazi wao na si viongozi serikalini wanaotunga sera ambazo zinaonekana kuwakandamiza walimu na taaluma yao. Tunasema hivyo kutokana na Serikali kutoshughulikia kero za muda mrefu za walimu.
Kwa nini Serikali inakataa kusikiliza vilio vya walimu? Moja ya sababu zinazotajwa kusababisha hali hiyo ni madai kwamba viongozi wanapeleka watoto wao kusoma nje ya nchi, huku watoto wa wananchi maskini wakisoma katika ‘shule’ zisizokuwa na madarasa, madawati, walimu wala vifaa vyenye ubora. Kudidimia kwa viwango vya elimu katika ngazi zote za elimu na kutokuwapo mfumo wa elimu endelevu ni kielelezo tosha cha kuwapo hali hiyo.
Ndiyo maana tunapata wakati mgumu kuelewa sababu zinazoifanya Serikali kutoona umuhimu wa kutafuta suluhisho la kudumu la madai ya walimu. Inashangaza kuona kwamba Serikali iliiahidi CWT kwamba mwezi uliopita ingelipa madai ya walimu yanayohusu malimbikizo ya mishahara, lakini imebadili ahadi hiyo na kusema italipa fedha hizo taratibu. Pamoja na vikao vingi vya majadiliano vilivyofanyika kutokana na maagizo ya Mahakama ya Kazi ya mwaka 2012, hakuna chochote kilichopatikana kutoka serikalini.
Serikali pia imeshindwa kupandisha walimu madaraja kwa kasi iliyotarajiwa. Hadi mwezi uliopita ni baadhi ya wilaya katika mikoa 12 ambako walimu wamepandishwa madaraja. Hii ni kwa sababu Serikali haikufanya maandalizi mazuri ya kuweka mfumo wa kutathmini utendaji kazi, hivyo kazi ya tathmini ya kupandisha walimu madaraja kuchelewa.
Majadiliano ya mishahara ya walimu yalitokana na mgomo wa walimu wa mwaka 2012, wakati Serikali ilikubali kulipa deni hilo na kuandaa utaratibu wa kupandisha walimu madaraja. Sasa miaka miwili imepita. Ndiyo maana tunaiona kauli ya Waziri wa Elimu na Mafunzo, Dk. Shukuru Kawambwa kuwa Serikali inaendelea kujadiliana na taasisi za fedha juu ya namna ya kulipa deni hilo, kuwa ni ulaghai usiohitajika katika kushughulikia matatizo nyeti kama hayo.
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa