Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mkazi
wa Mwananyamala Dar es Salaam, Sabrina Buruhani, anatuhumiwa
kumnyanyasa, mwanae wa kike na kutishia kumuua, hatua iliyolazimisha
mtoto huyo kuishi na mwalimu wake.
Unyanyasaji huo uliibuliwa kwenye kikao cha uongozi wa shule ya
Mchangani anakosoma mtoto huyo (jina linahifadhiwa), kilichohusisha
asasi ya utetezi wa haki na usawa kijinsia (Gewe) pamoja na wazazi
wake.
Mkutano huo ulifanyika shuleni hapo wiki hii na wazazi hao
walikubaliana binti huyo mwanafunzi wa darasa la tatu, mwenye umri wa
miaka nane aishi na baba yake.
Akiibua tuhuma, mwalimu wa binti huyo, Gaudensia Donatus, alisema
alilazimika kumchukua na kuishi naye kwa siku nne baada ya Sabrina
kutishia kumuua.
Aliwaambia wajumbe kuwa wiki iliyopita mtuhumiwa alifika shuleni
hapo akiwa na mwanae akifoka kuwa anamtafuta Denis, mwanafunzi wa
Mchangani aliyemtuhumu kuwa kila mara anachafua shati la binti yake kwa
wino.
“Aliingia shuleni bila kufuata utaratibu akitoa maneno makali
akiwa amempiga mwanae na kueleza kuwa anamtaka Denis amchape pia,”
alisema mwalimu huyo na kuongeza kuwa alikataa kutii maelekezo huku
akitishia kumuua mtoto wake.
Hata hivyo, alisema kutokana na hali hiyo, iliwalazimu
kumnyang’anya mtoto ili kuokoa maisha yake na baadaye alipelekwa kwa
shangazi yake mkazi wa Upanga na kumjulisha kilichotokea.
Alisema alipoelezwa kuhusu wifi yake, alidai amechoshwa na vitendo
vya mama huyo kwani alishawahi kumchukua mtoto huyo na kuwafanyia
vurugu nyumbani kwake.
Alisema madhumuni ya kumchukua mtoto huyo ni kuhakikisha anakuwa kwenye mazingira salama.
Mwakilishi wa Gewe, Asha Said alisema kuna haja ya mtoto huyo
kuulizwa iwapo anataka kuishi na baba yake au anapendelea kuishi na
mama.
Kwa upande wa baba mzazi Constant Saiboko, alikiambia kikao hicho
kuwa yupo tayari kumchukua mtoto wake na kumtafutia shule nyingine ya
bweni na hakubaliani na mateso yake.
Alieleza kuwa anafahamu anavyoteseka na aliwahi kumhamishia kwa
shangazi yake lakini mama huyo alikwenda kumfanyia vurugu jambo ambalo
hataki kuona likijitokea tena.
Sabrina alisema hayupo tayari kumtoa mwanae kwa kuwa anajua
hatamuona tena katika maisha yake lakini akataka kulipwa Sh 500,000 ili
amkabidhi kwa mzazi mwenzake.
“Endapo nitapatiwa 500,000 nipo tayari kumuachia mtoto huyo na
fedha hizo zitakuwa ni kama fidia ya kumlea,”alisema na Saiboko
aliahidi kuitoa fidia hiyo Julai mwaka huu kwani kwa sasa hana fedha
hizo.
Mkuu wa shule ya Mchangani, Janester Emilly, alikubaliana na
maamuzi yaliyofanywa na kuahidi kuwa atayasimamia ili kumuokoa mtoto
huyo.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment