Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Kutoka kushoto: Freeman Mbowe(Chadema), Profesa Ibrahim Lipumba(CUF) na James Mbatia(NCCR - Mageuzi)
Kadhalika wajumbe hao wamemkosoa Rais kuwa hakwenda kuzindua bunge
hilo bali kuzindua rasimu ya CCM na kudhalilisha maoni ya wananchi
kupitia Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Wawakilishi hao wakichambua hotuba ya Rais walisema hotuba ya juzi
imeonyesha dhahiri kutangaza rasmi kuvunja Muungano baina ya
Tanganyika na Zanzibar.
Wakizungumza na wanahabari mjini Dodoma, viongozi wa Ukawa walisema
hawako tayari kuona mawazo ya wananchi yakichakachuliwa kwa faida ya
chama tawala.
Mwenyekiti wa Ukawa, Profesa Ibrahim Lipumba alisema kuwa katika
hotuba yake, Rais Kikwete alitumia muda mwingi kuweka vitisho kuhusu
uanzishwaji wa muundo wa serikali tatu kuwa endapo utapitishwa, unaweza
kusababisha nchi kupinduliwa na jeshi huku akitoa maelekezo ya kuwapatia
Wazanzibar mamlaka zaidi ya kujitawala kama nchi inayojitegemea.
Kutokana na kauli hiyo, ni wazi kuwa Zanzibar itajitenga kutokana
na yenyewe kuwa na katiba inayoitambua kama taifa linalojitegemea.
“Sisi tulitarajia kwamba Rais atakuja kutuunganisha, badala yake
hotuba aliyoitoa ni ya kututenganisha na hatuwezi kukubali kutumiwa
kupitisha mambo wanayoyataka CCM badala ya Rasimu ya wananchi
iliyowasilishwa na Jaji Warioba,” alisema.
Alisema alichakachua takwimu za Tume ya Mabadiliko ya Katiba
kuhusu watu waliotoa maoni juu ya muundo wa Muungano na alitumia takwimu
zilizotolewa kwenye baadhi ya magazeti badala ya takwimu halisi za
Tume.
“Tumesikitishwa na kitendo cha Rais kutumia takwimu ‘alizookota’
kwenye gazeti la … (analitaja) na kudhalilisha rasimu ya katiba ambayo
yeye mwenyewe alianzisha mchakato wake,” alisema.
Alieleza kuwa badala ya kuzindua bunge hilo, alitumia muda mwingi
kusisitiza msimamo wa CCM kwa kupigia debe rasimu inayodaiwa kuwa
tayari imeandaliwa na chama hicho kitu ambacho hakupaswa kukifanya kama
Rais wa watu wote.
Profesa Lipumba alisema kama CCM walikuwa na Rasimu yao ya Katiba,
walipaswa kuitisha Mkutano Mkuu wa CCM kuijadili na siyo kuipeleka
kwenye bunge hilo ambalo ni chombo muhimu cha kujadili mustakabali wa
nchi.
Alisema hawatakuwa tayari kuona rasimu inayopaswa kujadiliwa ambayo
inatokana na maoni ya wananchi inawekwa pembeni na badala yake
inaingizwa CCM.
Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia alitahadharisha kuwa
endapo CCM itaendelea kuchezea mchakato wa katiba mpya itasababisha nchi
kuingia kwenye machafuko.
Alisema kuwa Rasimu ya Katiba iliyopatikana imetokana na maridhiano
ya Wazanzibar ambao waliunda serikali ya kitaifa, hivyo kutokana na
matamko ya Rais Kikwete ni dhahiri kuwa amewatukana Watanzania kutokana
na mawazo waliyoyatoa kwenye tume.
Mbatia alisema Rais Kikwete wakati akipokea rasimu ya kwanza na ya
pili pamoja na kwenye mkutano wa maridhiano na vyama vya kisiasa,
aliwataka viongozi wa kisiasa kuzingatia maslahi ya nchi badala ya
kuweka mbele itikadi zao za kisiasa katika kuhakikisha Tanzania inapata
katiba bora.
Lakini cha kusikitisha ni kwamba Rais Kikwete mwenyewe amekiuka
makubaliano hayo na kuingiza itikadi yake kwa kutetea hadharani msimamo
wa CCM na kupuuza maoni ya wananchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe alisema
kutokana na hotuba yake, Rais Kikwete ameweka misingi mibaya ya
upatikanaji wa katiba nzuri kwa kubeza maoni ya Watanzania.
Mbowe alitolea mfano kwa Mwanasheria Mkuu Mstaafu wa Kenya, Seneta
Amos Wako aliyesema serikali iliingilia na kuchakachua rasimu ya katiba
kwa kuingiza vifungu 13 ambavyo vilisababisha machafuko nchini humo.
“Rais na Chama chake cha CCM wasijidanganye kuwa wingi wao
utawasaidia kuchakachua rasimu na kupuuza maoni ya wananchi, tutapambana
ndani na nje ya bunge ili wananchi waweze kutendewa haki,” alisema
Mbowe.
Tundu Lissu kwa upande wake alisema licha ya kanuni walizopitisha
kukataza Rais asifanyiwe dhihaka, itabidi kanuni hiyo isitumike kwa kuwa
Rais mwenyewe ameanza kuwadhihaki wabunge na wananchi .
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment