Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MLINZI wa Kampuni ya Security Guard, Keiya Kapuka (28) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Ilala, kujibu mashitaka ya kunajisi mtoto wa miaka miwili. Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Munde Kalombola alidai mbele ya Hakimu Ester Mwakalinga kuwa Februari 9, mwaka huu, eneo la Mtaa wa Muheza wilayani Ilala, Kapuka alimnajisi mtoto wa miaka miwili.
Mshitakiwa alikana mashitaka na alirudishwa rumande baada ya kutokuwa na wadhamini. Kesi itatajwa Machi 13, mwaka huu.
Wakati huohuo, mkazi wa Buguruni, William Malinga (25) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Ilala kujibu mashitaka ya kukutwa na silaha.
Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Munde Kalombola alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Hassani Juma kuwa Februari 27 mwaka huu, eneo la Buguruni Chama wilayani Ilala, Malinga alikutwa na silaha aina ya Chinese na bunduki yenye risasi 8 bila kuwa na kibali.
Mshitakiwa alikana mashitaka hivyo na alirudishwa rumande hadi Machi 17, mwaka huu, kesi itakapotajwa tena.
Wakati huohuo Sophia Mwambe anaripoti kuwa, watu wawili Rajabu Sulemani (47) na Elinami Kimaro (29) wamefikishwa katika Mahakama wa Wilaya Ilala kwa shitaka la wizi.
Mwendesha Mashitaka Anunciath Leopold alidai mbele ya Hakimu Janeth Kaluyenda kuwa washitakiwa hao walitenda kosa hilo Februari 2, mwaka huu maeneo ya Ilala.
Alidai washitakiwa hao walivunja stoo na kuiba katoni 50 za viroba vyenye thamani ya Sh milioni 3.7, katoni 5 za baltika zenye thamani ya Sh 185,000, kompyuta moja aina ya HPA na printa, yenye thamani ya Sh 800,000 na pakiti 4 za zanzi zenye thamani ya Sh 64,000.
Pia, waliiba katoni 60 za Windhoek zenye thamani ya Sh milioni 3.4, katoni 4 za pombe ya kiroba aina ya jogoo zenye thamani ya Sh 340,000, vyote vikiwa na thamani ya Sh milioni 8.6 mali ya Alfred Lyimo.
Washitakiwa wamekana shitaka lao. Walirudishwa rumande na kesi itasomwa tena Machi 17, mwaka huu.
Chanzo;Habari Leo
0 comments:
Post a Comment