Home » » Moi yafungua kambi hospitali za mikoani

Moi yafungua kambi hospitali za mikoani

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Waziri wa Afya, Dk. Seif Seleman Rashid
 
Taasisi ya Magonjwa ya Mifupa na Fahamu (Moi), imefungua kambi maalum kwenye hospitali za mikoa kwa lengo la kukabiliana na mrundikano mkubwa wa wagonjwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Daktari Bigwa wa upasuaji wa kichwa, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu, Othman Kilolomo, alisema matatizo hayo yanazidi siku hadi siku na kusababisha msongamano mkubwa wa wagonjwa kwenye taasisi hiyo.

Dk. Kilolomo alisema kuwa ongezeko hilo linasababisha wagonjwa wengi kulala chini.

Kwa mujibu wa Dk. Kilolomo, kwa sasa taasisi hiyo inahudumia wagonjwa zaidi ya 600 ambao wengi wao hurudishwa tena wodini.

“Kwa mwezi tulikuwa tunawahudumia wagonjwa 600 lakini kwa sasa wamezidi na taasisi imeelewa," alisema.

Dk. Kilolomo aliongeza kuwa katika kukabiliana na mrundikano huo, madaktari bigwa wa taasisi hiyo wameanzisha kambi maalum mikoani kwa kushirikiana na kampuni ya Barrick African Gold ambayo madaktari hao wataendesha shughuli za upasuaji wa wagomjwa mbalimbali.

Alisema madaktari hao kuanzia leo watakuwa kwenye Hospitali ya Bugando jijini Mwanza na tayari wengine wapo Tanga, Iringa na Chimala mkoani Mbeya ambako wanaendelea na zoezi hilo.

Dk. Kilolomo alisema madaktari hao wataendesha huduma ya upasuaji wa kichwa, uti wa mgongo pamoja na kichwa kujaa maji, zoezi hilo litaaza leo mpaka Machi 28, mwaka huu na huduma hizo zitatolewa bure.

Naye Daktari Bigwa wa ubongo uti wa mgongo na mishipa ya fahamu, Hamis Shaaban, alisema kambi hiyo itakuwa kwenye Hospitali ya Mkoa wa Morogoro na kuwataka wazazi na hata wa mikoa ya jirani kuwapeleka watoto wenye matatizo hayo na watagharimiwa kila kitu ikiwamo chakula na malazi.

Dk. Shaabani aliongeza kuwa kambi ya Morogoro imedhaminiwa na kampuni ya mafuta ya Puma na kusisitiza kuwa ugonjwa wa mgongo wazi unatibika na kupona.

Katika hatua nyingine, Taasisi hiyo pia itaendesha huduma za  bure za upasuaji kwa ajili ya matatizo ya mgongo wazi, ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu kwenye kambi itakayokuwa Morogoro kuanzia Aprili 4 hadi 8, mwaka huu.
 
SOURCE: NIPASHE

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa