Na Sophia Yamola, Bagamoyo
“Mara ya mwisho kwenda hospitali ilikuwa mwaka 2002 ambapo niliambiwa nitafute shilingi milioni tano kwa ajili ya matibabu. Kwa kuwa sikuwa na uwezo kutokana na umasikini nilio nao, niliamua kumuachia Mungu”
Ndivyo anavyosema Ngawaji Said, mkazi wa Bagamoyo mkoani Pwani kutokana na “ugonjwa” uliomsababishia kuwa na uvimbe uliomsababishia nyama kubwa iliyofunika uso na kuning’inia hadi mabegani huku ikimfanyia mateso tangu akiwa na umri wa miaka 10.
Anasema katika mazungumzo na mwandishi wa makala haya katikati ya juma lililopita akisistiza kuwa, tatizo hilo ambalo limekuwa likiongezeka kadiri siku zinavyokwenda, amekuwa nalo kwa kipindi cha takriban miaka 30.
Mwandishi wa makala haya akiwa na Ngawaji
Ngawaji anayesema hali hiyo imemfanya aishi maisha magumu na ya mateso na kuamua kumtegemea Mungu pekee, anasema wazazi wake walifariki miaka 20 iliyopita.
Tangu hapo anasema, amekuwa akiishi maisha ya tabu kutokana na hali ya umaskini inayomfanya ajione hana thamani tena mbele ya jamii kwa kukosa msaada toka kwa jamii kiasi cha kufikia kuishi na pengine, kufa katika mateso huku ndugu zake wengi pia wakiwa katika umaskini mkubwa.
Katika mazungumzo na Dira ya Mtanzania nyumbani kwake katika kijiji cha Zinga kilichopo wilayani Bagamoyo katika Mkoa wa Pwani katikati ya juma lililopita, Ngawaji tatizo lake lilianza akiwa na umri wa miaka 10 alipoota kijipele kichwani.
Anasema kwa huzuni kuwa, kadiri alivyokua, ndivyo kipele hicho nacho kilivyokua na kuongezeka uvimbe kiasi kwamba, sasa amefikia hatua hiyo anayosema, kama jamii haitaiona na kuamua kumsaidia, atakufa na kuzikwa nayo.
“Hata sijui ni ugonjwa gani unanisumbua japo kuwa madaktari waliniambia naweza kupona endapo nitafanyiwa vipimo vya kina na kupata matibabu. Unajua tatizo kubwa limekuwa ni fedha; sina uwezo wa kuzipata kutokana na hali ya umaskini nilio nao,” anasema Ngawaji.
Anaongeza, “Unajua dada yangu (mwandishi) imefikia hatua najiona kama mtu tofauti na wengine kwa jinsi nilivyo na jamii inayonizunguka; kila mtu ananichukulia anavyoona yeye….”
Anasema mnamo miaka ya 90, alikwenda katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na kupatiwa matibabu ya awali, ingawa hakuwa amefanyiwa vipimo kubaini chanzo cha tatizo linalomsumbua.
Mwaka 2002 alibidi arudi tena hospitalini ambako walimwambia aende Hospital ya CCBRT iliyopo Msasani jijini Dar es Salaam kwa sababu kuna wataalamu wazuri ambao watampatia huduma kutokana na ugonjwa alio nao.
Alisema hata alipofika katika hospital hiyo hawakumpatia huduma yoyote iliyostahili kutokana na kutokuwa na fedha ambako walimwambia akatafute fedha kiasi cha milioni tano ndio atafanyiwa vipimo vya ugonjwa unaomsumbua.
“Umaskini mbaya ndugu zangu nigekuwa na fedha nisingekuwa nateseka na ugonjwa huu hadi leo toka walivyoniambia nikatafute fedha kiasi hicho cha shilingi milioni tano, sikuwa na jinsi kwa sababu tayari wazazi wangu walikuwa wameshafariki hata ndugu zangu wawili ambao nimezaliwa nao tumbo moja hawana uwezo wa kupata hata laki tano.”
“Hivyo ilinilazimu kumuachia Mungu ugonjwa wangu ambao umekuwa ukiongezeka kila ninapokuwa” alisema Ngawaji.
Anaongeza kuwa, toka mwaka 2002 aliokwenda CCBRT na kuambiwa gharama za matibabu ya tatizo lake yanahitaji shilingi 5,000,000, alikata tamaa na kuamua kutulia .
“Nafikiri sasa gharama itakuwa imeongezeka kwa sababu toka kipindi hicho hadi sasa ni zaidi ya miaka 12 sasa imepita,” anasema.
“Kama unavyojua, kila siku gharama zinaongezeka hivyo usishangae nikienda tena hospitalini wakaniambia gharama nyingine au natakiwa nikafanyiwe matibabu nje ya nchi kutokana na ugonjwa wangu kuwa wa muda mrefu,” alisema Ngawaji.
Pamoja na mateso anayoyapata ambayo yanafanya kichwa chake kuwa kizito kutokana na ugonjwa huo, Ngawaji hana mke wala mtoto kutokana na hali aliyo nayo ambayo imemfanya asioe.
“Kwa hali niliyo nayo unafikiri ni nani atakubali kuolewa na mimi? Sina mke wala mtoto, na hata kama ningeoa nigemhudumia vipi huyo mwanamke kutokana na hali yangu ni mwanamke gani atakubali kuolewa na mimi?” anasema Ngawaji huku akionesha hamu ya kuishi na mwanamke.
Anasema endapo atapatiwa matibabu ambayo kimsingi yamekuwa ndoto kwake, jicho lake la kushoto halitakuwa na uwezo wa kuona kwa sababu limeshaharibika kutokana na ugonjwa huo.
“Hata kama nitapatiwa matibabu ya kuondoa huu ugonjwa, uwezekano wa jicho langu la kushoto kuona haupo tena hivyo nitaendelea kutumia jicho moja ambalo nalo linazidi kuvutwa na huu ugonjwa” alisema Ngawaji.
Ngawaji ambaye anaishi kwenye chumba kimoja alichopewa na msamaria mwema, amekuwa akijipatia kipato kwa kuchajisha simu, ambapo simu moja huchajisha kwa shilingi 200 na kwa siku moja huchaji simu nane au kumi na kupata shilingi 1000.
“Kila kukicha maisha yangu kwa kweli yanategemea kudra za Mwenyezi Mungu, kwa sababu kipato changu kwa siku ni shilingi 1000, wakati mwingine wateja wa kuchajisha simu hawalete hivyo kujikuta nikiambulia patupu na fedha hiyo haikidhi mahitaji yangu ya kila siku,” anasema.
Ngawaji anawaomba wasamaria wema na wote wanaoguswa na tatizo lake, wajitokeze kumsaidia kwa hali na mali kwa kadiri ya uwezo wa mtu au kikundi, ili atafute matibabu.
Anasema anayeguswa na kupenda kumsaidia kupata matibabu na huduma mbalimbali muhimu na za lazima kwake, afanye hivyo kupitia simu yake ya mkononi namba0659 764461 Akaunti Namba Ya Benki 'NMB' 21010002737
“naamini ndugu zangu Watanzania na hata wengine wasio Watanzania wenye mapenzi mema na wanaoguswa, watanisadia kila mtu kwa mchango wa uwezo wake.”
Mwandishi wa Makala haya anapatikana kwa 0715 221208
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment