Home » » Uhamishaji wa kituo cha daladala Ubungo wasuasua

Uhamishaji wa kituo cha daladala Ubungo wasuasua

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Msemaji wa Manispaa ya Kinondoni,Sebastian Mhowera.
 
Uhamishaji  wa kituo cha mabasi ya daladala cha Ubungo jijini Dar es Salaam kwenda kwenye eneo jipya lililopo nyuma ya jengo la Mawasiliano Towers, bado umekwama kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ya fidia.
Kwa mujibu wa serikali, zoezi hili ambalo linafanyika kwa ajili ya kupisha kwa mradi wa mabasi yaendayo kasi (Dart), lilitakiwa kukamilika mwanzoni kwa Februari, mwaka huu.

Akizungumza na NIPASHE, Msemaji wa Manispaa ya Kinondoni, Sebastian Mhowera, alisema  fidia, ni moja ya sababu zinazochelewesha kukihamisha kituo cha Ubungo kwenda eneo jipya.

“Kuna nyumba ambazo inabidi zivunjwe ili kupisha upanuzi wa barabara inayoingia na kutoka katika kituo kipya ikiwamo hoteli ya City Style, lakini hatuwezi kufanya upanuzi huo bila ya kuwalipa fidia wenye mali, kama sheria inavyotaka,” alisema.

Mbali na fidia, Mhowera alisema sababu nyingine inayocholewesha kuhamisha kituo cha Ubungo kwenda kwenye eneo jpya, lililopo hatua chache toka babara ya Sam Nujoma au ile ya Shekilango katika eneo la Mugabe ni ya lami.

Alisema barabara inayoingia na kutoka katika kituo kipya, ni lazima iwekewe lami kwanza kabla ya kuanza kutumika.

NIPASHE ilitembelea eneo la kituo kipya na kukuta limekamilika kwa asilimia kubwa ikiwamo kuzungushiwa fensi, vibanda vya ndani vya kusubiria, mageti ya kuingia na kutoka pamoja na baadhi ya miundo mbinu kama vyoo.

Hata hivyo, eneo hilo lote jipya pamoja na  barabara ya kuingia na kutoka havijawekewa lami.

Mwishoni mwa Januari, mwaka huu, baadhi ya vyombo vya habari vilimunukuu Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuph Mwenda, akiahidi kwamba kituo kipya kingeanza kutumika mwishoni mwa mwezi huo.

Alisema waliamua kuhamisha kituo cha daladala cha Ubungo kwenda katika eneo jipya, kutokana na ufinyu wa eneo hilo uliochangiwa na mradi wa Dart.

Aidha alisema, wafanyabiashara ndogo ndogo hawataruhusiwa kuendesha shughuli zao katika eneo hilo, kwa kuwa si salama kwao.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa