Zikiwa
zimebaki siku chache Tanzania iungane na mataifa mengine kuadhimisha
siku ya Wanawake duniani , Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Mh. Saidi Meck
Sadiki ameeleza kuwa ipo haja ya jamii, Asasi za kiraia na zile za
kidini kushiriki kikanilifu katika kuweka mikakati ya kukabiliana na
changamoto mbalimbali zinazowakabili wanawake nchini.
Akizungumza
na waandishi wa habari Jana jijini Dar es salaam maadhimisho ya Siku
ya Wanawake Duniani yatakayofanyika tarehe 8 mwezi huu Mh. Sadiki Meck
Sadiki ameeleza kuwa licha ya mchango mkubwa wanaoutoa katika maendeleo
ya taifa wanawake wanakabiliana na changamoto mbalimbali kutoka katika
jamii inayowazunguka.
Amesema
licha ya wanawake kuwa na jukumu la kutunza familia, kuendesha shughuli
za uzalishaji wa bidhaa na huduma mbalimbali kutokana na shughuli za
ujasiriamali bado wanakabiliwa na changamoto za maradhi, vifo
vitokanavyo na uzazi, kupigwa, kutukanwa, kutelekezwa, kubakwa,
kuandamwa na vitendo vya ukeketaji na mauaji ya vikongwa.
Amezitaja
changamoto nyingine kuwa ni pamoja na kunyimwa haki ya kumiliki mali,
kutoshirikishwa na kutopewa haki sawa katika ngazi za maamuzi na
kuongeza kuwa wakati umefika sasa kwa jamii kutambua na kuthamini
mchango walio nao kijamii, kisiasa na kiuchumi kwa kuwapa wanawake fursa
sawa katika nyanja zote.
“
Siku ya Wanawake duniani inaongozwa na Kauli mbiu isemayo, Chochea
Mabadiliko Kuleta Usawa Kijinsia , ujumbe huu unaelimisha na kuhamasisha
jamii, Serikali, Asasi za Kiraia na za Kidini kutambua umuhimu wa
kushirikiana wanaume na wanawake katika ngazi zote za maendeleo”
Ameeleza
kuwa jiji la Dar es salaam litaungana na maeneo mengine nchini katika
kuiadhimisha siku hiyo muhimu kwa maadhimisho makubwa yatakayofanyika
katika uwanja wa Mwembeyanga katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke
huku mgeni rasmi akiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa Hawa Ghasia.
Katika
hatua nyingine Mh. Meki Sadiki amewataka wakazi wa jiji la Dar es
salaam hususan wale wanaoishi katika maeneo hatarishi yanayokumbwa na
mafuriko mara kwa mara kutii taarifa ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania
kwa kuondoka katika maeneo hayo kufuatia mvua kubwa zinazoendelea
kunyesha nchini ili kuepuka madhara yanayoweza kuepukika.
Akitoa
taarifa kuhusu mikakati ya kukabiliana na majanga yanayoweza kutokea
wakati wa msimu wa mvua kama ilivyotabiriwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa
Mh. Meck Sadiki ameeleza kuwa tayari serikali imejipanga chini ya
kitengo cha Maafa cha Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuwa na kikosi kazi
kinachohusisha vikosi vya ulinzi na usalama vya majeshi ya Tanzania.
Ameeleza
kuwa serikali kwa kuthamini umuhimu wa maisha ya raia wake hasa wale
waishio mabondeni imekuwa ikitoa taarifa za kuhama mapema lakini baadhi
yao hugoma kuyahama maeno yao na pindi wanapoondolewa kwa nguvu huamua
kwenda mahakamani kuishitaki serikali.
“Mara
nyingi tumekuwa tukiwataka mara kwa mara wale wote wanaoishi bondeni
kuhama sio tu wakati wa msimu wa mvua lakini wenzetu wamekua wakiona
suluhisho lao ni kukimbilia mahakamani jambo ambalo linasababisha
mahakama kusimamisha zoezi letu kama tunavyojua serikali yetu inaheshimu
uhuru wa mahakama”
Kuhusu
kesi zilizopelekwa mahakamani kuhusiana na zoezi la kuwaondoa wananchi
wanaoishi katika bonde la mto Msimbazi amesema tayari kuna kesi nne
zinazoendelea kushughulikiwa na tayari Manispaa ya Ilala imeshinda kesi
moja.
Ametoa
wito kwa wananchi kuchukua tahadhari katika kipindi hiki ikiwemo kutoa
taarifa za matukio yanayohatarisha maisha na kujenga tabia ya
kushirikiana katika kutatua changamoto zinazoweza kujitokeza pia kutoa
taarifa kwa mamlaka husika pindi wanapoona baadhi ya watu wanajenga
katika maeneo yasiyoruhusiwa.
0 comments:
Post a Comment