Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Afisa Elimu wa Sekondari Manispaa ya Ilala,Violet Mlowosa.
Katika matokeo hayo yaliyotangazwa Februari 21, 2014 na Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Dk. Charles Msonde, Mvuti ilikamata nafasi ya tano miongoni mwa orodha ya shule kumi zilizofanya vibaya. Katika wanafunzi wao 62 waliotakiwa kufanya mtihani huo, watatu hawakufanya kabisa, matokeo ya wanafunzi 15 yamezuiwa kwa sababu mbalimbali, mmoja amefaulu kwa kiwango cha daraja tatu, watatu waliambulia daraja la nne huku wengine 40 wakifeli vibaya kwa kupata daraja sifuri. Kwa ujumla, Mvuti ilishika nafasi ya 3,251 kati ya shule 3,256.
Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE umebaini kuwa sababu nyingine zinazochangia kufanya vibaya kwa wanafunzi wa shule hiyo tyenye namba za usajili S.1680 ni pamoja na ukosefu wa vitabu vya kiada na ziada, uhaba wa maji na pia kuwapo kwa baadhi ya walimu wanaofanya kazi kwa shingo upande kutokana na kutolipwa madai yao mbalimbali kwa muda mrefu, yakiwamo ya malimbikizo ya nyongeza za mishahara baada ya kupandishwa madaraja.
UWEZO MDOGO
Uchunguzi umebaini kuwa licha ya changamoto nyingi zilizopo katika shule hiyo mojawapo ya kata ya Msongola iliyoanzishwa mwaka 2006, pia kuna tatizo kubwa la kuwapo kwa wanafunzi wasioandaliwa vyema kukabiliana na mitihani ya kidato cha nne.
Kwa mfano, chanzo chetu kimeithibitishia NIPASHE kuwa miongoni mwa wanafunzi waliofanya mtihani uliopita wa kidato cha nne na kuipa matokeo mabaya shule hiyo, ni watatu tu ndiyo waliofaulu wakati walipofanya mtihani wa taifa wa kidato cha pili. Idadi hiyo inamaanisha kuwa takriban asimilia 95 ya waliopaswa kufanya mtihani huo (katika wanafunzi 62), walifeli na hivyo hawakuwa na sifa ya kuendelea kidato cha tatu na mwishowe kufanya mtihani.
“Hawa walipokuwa kidato cha pili walifeli pia na kutofikia wastani wa chini wa alama 30... hata hivyo, walisalimika baada ya serikali kuamuru kuwa wao na wengine wengi nchini kuendelea na masomo. Hivyo utaona kuwa matokeo haya hayashangazi sana,” chanzo kimoja shuleni hapo kiliiambia NIPASHE.
Uchunguzi zaidi umebaini kuwa hata watoto wanaoripoti kwenye shule hiyo baada ya kufaulu darasa la saba, wengi wao huwa ni wazito sana darasani na baadhi huwa hawajui hata kusoma na kuandika.
Kwa mfano, imeelezwa kuwa asilimia 70 ya wanafunzi zaidi ya 180 walioripoti katika shule hiyo baada ya kufaulu darasa la saba mwaka 2011 walibainika kuwa hawajuyi kusoma wala kuandika na hivyo kuwapa wakati mgumu walimu.
“Wewe mwenyewe hebu fikiria ndugu yangu, kama mtoto hajui hata kusoma na kuandika, mwalimu utawezaje kumfundisha Physics, Geography, Historia, Kemia na masomo mengine ya sekondari? Ni wazi kwamba hakutakuwa na muujiza... mwisho wa siku watoto wa aina hii ni lazima watafeli tu,” kilieleza chanzo chetu.
Aidha, imeelezwa vilevile kuwa Mvuti imekuwa ikisimuliwa kwa sifa mbaya kuhusu taaluma na matokeo yake, hata wanafunzi wazuri wachache wanaokuwa nao hujikuta wakihamishwa na wazazi wao na hivyo kuwapunguzia uwezekano wa kupata matokeo mazuri.
“Hata hivi sasa, katika kidato cha nne wamebaki wanafunzi saba tu. Wengi wazuri walishahamishwa, waliobaki kama 200 hivi walifanya mtihani wa taifa wa kidato cha pili. Wwengi wakafeli na kujikuta wakiachia ngazi,” chanzo chetu kiliongeza.
USAFIRI, NJAA KALI
Shule ya Mvuti iliyoko katika eneo la ukubwa wa ekari 48, iko katika eneo lililoko nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam. Kwa bahati mbaya, baadhi ya wanafunzi na walimu hutoka katika maeneo ya mbali ndani ya manispaa ya Ilala, yakiwamo ya Tabata, Buguruni.
Kwa sababu hiyo, wapo wanafunzi wanaolazimika kupanda mabasi sita kwa siku na kisha kulazimika kutembea kwa miguu umbali wa zaidi ya kilomita nane kwa safari za kwenda shule na kurudi kila uchao.
Kwa mfano, mwandishi alielezwa kuwa mmoja wa wanafunzi wanaoishi Tabata hulazimika kuamka saa 10:00 alfajiri na kuanza safari kwa kupanda mabasi ya kwenda Buguruni, kisha hushuka na kupanda Gongolamboto, baadaye husuka na kupanda mabasi ya Chanika, wakifika huko huteremka na kupanda tena mabasi ya kuelekea Mvuti kabla ya kuanza upya safari kwa kutembea kwa miguu umbali wa takriban kilomita nne ili kufika shuleni.
Mwandishi alishuhudia baadhi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza na cha pili wakisaidiwa kwa kupewa lifti kwenye malori ya kubebea mchanga huku wengine wenye fedha wakilazimika kukodi pikipiki ambazo huwatoza nauli ya Sh. 1,500 kwa safri moja ya kutoka kwenye kituo cha mabasi cha Mvuti hadi shuleni.
"Mabasi ya moja kwa moja kwenda Mvuti ni shida. Wengi hulazimika kupanda mabasi kati ya matatu na manne kwa safari moja na matokeo yake hufika shuleni wakiwa hoi kwa uchovu. Wapo walimu pia wanaokaa Mbezi na maeneo mengine ya mbali na Mvuti. Matokeo yake, mara nyingi wanafunzi na walimu hujikuta wakichelewa kwa pamoja.
Wapoa wanafunzi pia hukabiliwa na njaa kali mchana kwa sababu shule haitoi chakula. Katika mazingira kama haya, ni vigumu wanafunzi kuzingatia masomo na kufaulu katika mitihani yao ya mwisho,” chanzo kilieleza.
NIPASHE imebaini kuwa wanafunzi wenye ahueni kuhusiana na adha hii ni wale wanaokaa kwenye mabweni ya shule hiyo yanayotumiwa na wasichana wasiozidi 100. Kwa ujumla, shule hiyo inayokabiliwa pia na tatizo kubwa la ukosefu wa maji, ina wanafunzi 357.
VIFAA, UONGOZI
Uchunguzi wa NIPASHE umebaini vilevile kuwa shule ya Mvuti ina tatizo kubwa la ukosefu wa vitabu na pia uongozi. Hakuna vitabu vya kutosha vya kiada wala ziada kwa masomo yote, hivyo walimu hujikuta katika wakati mgumu.
Shule hiyo pia haina mkuu wa shule tangu Agosti mwaka jana. Mwalimu aitwaye Wilfred Sanga ndiye hukaimu na licha ya kujituma sana, bado hujikuta akikwama katika baadhi ya maeneo kwa vile wapo walimu wasiotii maelekezo yake kwa vile wanajua kuwa yeye anakaimu tu na wala hana mamlaka kamili.
MKUU WA SHULE, MWENYEKITI WA BODI
Kaimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mvuti, Sanga, alisema kuwa zipo sababu nyingi zinzotokana na changamoto kadhaa zinazowakabili.
“Ni kweli, yapo baadhi ya matatizo yanayokwaza maendeleo ya shule yetu kitaaluma. Hata hivyo, mimi siyo msemaji... hii nafasi (ya mkuu wa shule) ninakaimu tu na hivyo unisamehe. Tuna vikao tulifanya na hivyo mtafute mwenyekiti wa bodi anaweza kukueleza,” alisema Sanga.
Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Mvuti, Benedict Ndalahwa, alisema wanakabiliwa na changamoto nyingi na kwamba sasa, baada ya kuitisha kikao cha dharura cha bodi kilichofanyika Machi Mosi ili kubaini chanzo cha kufanya vibaya na kutafuta njia za kuepukana na janga hilo, tayari wameazimia mambo mengi ambayo wanaamini kuwa wakiyatekeleza kwa asilimia mia moja, shule hiyo itapiga hatua haraka na kuwa mkiongoni mwa shule zinazofanya vizuri kwenye Manispaa ya Ilala.
"Shule haikuwa na bodi kwa takriban miaka miwili sasa. Na mbaya zaidi haina mkuu wa shule aliyethibitishwa tangu Agosti mwaka uliopita. Mimi nimeanza kuwa mwenyekiti (wa bodi) Februari 15... hata mwezi sijatimiza.,” alisema. Alizitaja baadhi ya changamoto watakazoketi na wazazi ili kuzitafutia dawa kuwa ni pamoja na usafiri, chakula kwa wanafunzi na vitabu.
“Ni kweli kuna changamoto nyingi. Hata hivyo, tumegundua shule haina tatizo la walimu. Ni kwa sababu hadi sasa wapo walimu 24, kati yao watano wakiwa ni wa masomo ya Sayansi. Tutafuatilia zaidi ili kuona shule inapata mkuu wake na siyo kaimun kwa kipindi kirefu kama ilivyo sasa.
Hili litasaidia kuongeza uwajibikaji miongoni mwa walimu. Pia tutaomba serikali ifanyie kazi madai ya kuwapo kwa malimbikizo mbalimbali,” alisema Ndalahwa.
AFISA ELIMU ILALA
Afisa Elimu wa Sekondari Manispaa ya Ilala, Violet Mlowosa, alikiri kuwa ni kweli shule hiyo (Mvuti) inakabiliwa na changamoto nyingi, lakini anaamini kuwa kutokana na mwenendo walio nao sasa, ni wazi kwamba watabadilika na kufanya vizuri sana katika miaka michache ijayo.
“Jina la Mkuu wa Shule watalipata wakati wowote kuanzia wiki ijayo, kwahiyo hili haliwezi kuwa tatizo tena. Walikuwa hawana bodi kwa mudfa mrefu (zaidi ya miaka miwili), lakini sasa wanayo na kadri ninavyoona, kuna dalili kwamba sasa watakuwa wakifanya vizuri,” alisema.
Mlowosa alieleza zaidi kuwa hata hivi sasa, matokeo yao ya kidato cha pili yamedhihirisha kuwa wameanza kuwa na mwelekeo mzuri na kilichobaki kwao ni bodi ya shule kuketi na wazazi na kuangalia namna ya kumaliza tatizo la usafiri na chakula kwa wanafunzi ili hatimaye kuinua kiwango cha ufaulu.
“Matokeo yao kidato cha pili yanaonyesha kuwa mwaka 2011 walishika nafasi ya 303 katika shule 304 (za Dar), mwaka 2012 wakashika nafasi ya 304 katika shule 304 lakini mwaka 2013 wakapanda na kushika nafasi ya 220 katika shule 304... wameanza kuwa katika mwelekeo mzuri, wazazi wakubali kushirikiana na bodi katika kumaliza tatizo la usafiri na chakula na baada ya hapo naamini watafanya vizuri zaidi,” alisema Mlowosa.
Kuhusiana madai kwamba wanafunzi wengi wa kidato cha kwanza huripoti Mvuti wakiwa hawajui kusoma wala kuandika, Mlowosa alisema kuwa hilo haliko mikononi mwao.
“Mipango ya baadaye ni pamoja na kuona kuwa shule za aina hii (Mvuti) zinaongezewa mabweni... hata sasa, wale wanaokaa bwenini Mvuti hufanya vizuri zaidi kuliko wengine,” alisema Mlowosa.
SOURCE:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment