Home » » Sumaye: Watanzania tuongeze ari ya kutunga, kusoma vitabu

Sumaye: Watanzania tuongeze ari ya kutunga, kusoma vitabu

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Waziri Mkuu Mstaafu,Frederick Sumaye.
 
Watanzania wametakiwa kujibidiisha katika uandishi wa vitabu, ili kuwezesha utunzaji wa kumbukumbu muhimu za taifa kwa vizazi vinavyokuja.
Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, alitoa rai hiyo juzi jijini Mwanza, alipokuwa akizungumza kwenye uzinduzi wa kitabu kinachoitwa ‘Kufurahia ndoa’, kilichotungwa na wachungaji Zakayo na Carol Evelyn Nzogere.

Alisema si Watanzania wengi wanaoandika vitabu na hali hiyo hufanya kumbukumbu nyingi za mambo ya zamani kupotea, hali ambayo huifanya jamii iliyozaliwa baada ya jambo hilo kutokulifahamu.

“Hiki ndicho walichokifanya wachungaji hawa. Wameona kuna jambo lenye umuhimu kwa jamii wakaamua kukiandikia kitabu ili watu wafaidike na hayo waliyoyaandika humo,” alisema.

Alisema zaidi ya kumbukumbu, vitabu vinafundisha mambo mengi ya kuisaidia jamii katika taaluma mbalimbali au medani za kawaida za maisha.

Sumaye alisema kitabu hicho kitasaidia kupunguza tatizo linalozidi kukua nchini kuhusu ndoa nyingi kutetereka na hatimaye kuvunjika.

“Kama tunavyojua ndoa ni tendo takatifu lililoagizwa na Mwenyezi Mungu mwenyewe wakati wa uumbaji wake. Ndoa zinapotetereka au kuvunjika kuna mambo kadhaa yanaweza kutokea na huwa yanatokea katika maisha ya kila siku,” alisema.

Alitoa mfano wa matatizo hayo kuwa ni chuki baina ya wanandoa au waliokuwa wanandoa jambo ambalo wakati mwingine husababisha hata mauaji.

Mengine ni maambukizi ya magonjwa ya zinaa na Virusi Vya Ukimwi (VVU) kutokana na kujihusisha na kuwa na uhusiano wa kimapenzi nje ya ndoa.
SOURCE: NIPASHE

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa