Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WANAFUNZI
wanaosoma darasa la saba katika shule za msingi zilizofanya vibaya
kwenye matokeo ya mwaka jana na kushika nafasi za mwisho wilayani
Tunduru, wamesema hali hiyo inachangiwa na wazazi kuwashinikiza wajaze
majibu ya uongo kwenye mitihani yao ya mwisho, ili wafeli kwa lengo la
kuwanusuru na mkono wa sheria iwapo watafaulu na kushindwa kuwapeleka
sekondari.
Wanafunzi hao walitoa kauli hiyo mbele ya Mkuu wa Wilaya
ya Tunduru, mkoani Ruvuma, Chande Nalicho, alipofanya ziara ya
kushtukiza ili kujionea hali ya ufundishaji katika Shule za Msingi za
Machemba na Mbatamila ambazo zilifanya vibaya kwenye mtihani wa darasa
la saba.
Baadhi ya wanafunzi hao walimwambia mkuu wa wilaya kuwa chanzo cha wao kufeli mitihani ni wazazi na walezi.
Baadhi
ya wanafunzi hao, Alli Machemba, Amina Mohamedi, walielekeza lawama zao
kwa wazazi wao wakidai wanawashinikiza wajibu majibu ya uongo ili
kuwanusuru na mkono wa sheria.
"Chanzo cha kufanya vibaya katika
matokeo hayo ni wazazi na walezi wetu," alisisitiza mmoja wa wanafunzi
hao na kuongeza kuwa inapotokea wanafunzi wakafeli wazazi hao huwafanyia
sherehe kwa lengo la kuwapongeza.
Akitoa ushuhuda wa matukio hayo
aliyekuwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Machemba, Namkanda Alli,
alikiri kuwa hali hiyo ipo na kwamba ni moja ya sababu iliyomfanya aamue
kuachia nafasi ya ukuu wa shule kutokana na kukosa ushirikiano kutoka
kwa wazazi na walezi.
Alisema mwaka 2012 katika shule hiyo
alifaulisha wanafunzi 35, lakini alijikuta akiachia nafasi hiyo kutokana
na kukosa ushirikiano kutoka kwa wazazi na walezi, kwani wakati
mwingine walimkejeli.
"Nilichukua uamuzi wa kuachia madaraka hayo
ili nirudi darasani ili niondokane na masimango hayo," alisema Alli na
kuongeza; " Wazazi na walezi walikuwa wakinifuata na kunihoji kwanini
najifanya mwalimu bora."
Diwani wa Kata ya Kidodoma, Seif Yusiph,
pamoja na kikundi cha vijana sita waliohitimu shahada ya kwanza katika
Chuo Kikuu cha Dodoma wanazunguka kwenye kata za wilaya hiyo kuhamasisha
wazazi na wanafunzi ili watambue umuhimu wa elimu.
Wahitimu wa
shahada hiyo ya kwanza wanaozunguka na diwani huyo, ni Musa Lionga,
Rashid Mapunda, Mariam Mtelela, Geres Mbena, Gaibu Rashid.
Walisema
sababu zinazotolewa na wazazi hao si za kweli isipokuwa ni kutaka
kuwaangamiza watoto wao kimaisha. Walisema haiwezekani mzazi aseme hana
uwezo wa kulipa ada ya sh.20,000 kwa mwaka, wakati kila mwaka wanaongeza
wake.
Kwa upande wa Mtawala wa Jadi wa kabila ya Wayao (Sultani
Mataka wa 16) alilaani wazazi wanaohamasisha watoto hao kufeli mitihani
yao ili kuwanusuru sheria isichukue mkondo wake.
Awali akitoa
taarifa ya maendeleo ya taaluma katika Shule ya Msingi Machemba, Mwalimu
Mkuu wa shule hiyo, Ramji Mbawala, alisema shule yake ilifaulisha
watoto wote katika matokeo ya mwaka 2013.
Kwa matokeo hayo alisema shule hiyo ilishika nafasi ya 133 kati ya 137 zilizopo wilayani humo.
Akizungumzia
hali hiyo kwa niaba ya Ofisa Elimu Shule za Msingi wilayani humo,
Christantusi Haule, alisema visingizio vinavyotolewa na wazazi havina
ukweli wowote.
Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Nalicho alikemea tabia ya
utoro uliokithiri miongoni mwa wanafunzi pamoja na wazazi ambao
hawachukui hatua zozote kwa watoto wao wanapofanya vibaya.
"Kuanzia
sasa ni marufuku wazazi kuwafanyia sherehe wanafunzi wanaofeli,"
alisisitiza Nalicho na kuongeza kuwa mtu atakayekaidi agizo hilo sheria
itafuata mkondo wake.
Alisema hata wakifanya kwa kificho watagundulika tu kwa vile Serikali ina mkono mrefu.
Chanzo;Majira
0 comments:
Post a Comment