Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Juzi tarehe 18/03/2014 Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini
Jaji Joseph Sinde Warioba aliwasilisha kwenye Bunge maalum la Katiba
rasimu ya pili ya katiba.
Toka awasilishe rasimu ile bungeni , kumekuwa na maombi mengi sana ya
kutaka kujua kama msimamo wa CCM juu ya baadhi ya mambo hasa muundo wa
muungano bado ni uleule.
Kwasababu ya maombi hayo CCM imeona bora kueleza kwa mara nyingine tena
msimamo na imani ya CCM juu ya swala zima la Muungano na muundo wake.
Kimsingi CCM ndio waasisi wa Muungano huu wa Tanganyika na Zanzibar. CCM
inamasilahi makubwa na mapana na Muungano huu kama waasisi pengine
kuliko taasisi nyingi ndani na nje ya nchi yetu.
Bado CCM inaamini changamoto za Muungano huu suluhisho lake sio kubadili
muundo wa Muungano bali ni kuufanyia maboresho muundo wa muungano
tulionao wa serikali mbili. Hivyo basi CCM bado inaamini muundo bora
kwasasa utakao dumisha muungano wetu ni muundo wa SERIKALI MBILI.
Kwakuwa kazi ya Warioba na Tume yake sasa imekwisha rasmi, kuisha kwa
kazi yao ni mwanzo wa awamu nyingine ya mchakato huu. Mwisho wa kazi ya
Tume sio mwisho wa mjadala juu ya Katiba tuitakayo bali ni mwanzo wa
awamu nyingine ya mjadala mpana na maboresho kama sio marekebisho ya
kuondoa mapungufu kwenye rasimu iliyowasilishwa.
Mwanzo wa awamu hii nyingine ni furusa nzuri ya kupima kama kweli
yaliyomo kwenye rasimu na maelezo ya ziada yaliyotolewa na Jaji Warioba
yana akisi maoni ya Watanzania walio wengi.
CCM ina amini awamu mbili zilizobaki kwakuwa zinahusisha wawakilishi
wa wananchi kupitia Bunge maalum la Katiba, na hatimaye itawahusisha
wananchi wenyewe moja kwa moja kupitia kura yao, zitatumika vizuri
kutupa ni nini hasa matakwa ya Watanzania juu ya Katiba waitakayo na sio
maoni au matakwa ya wachache.
Wakati haya yote yakiendelea CCM bado tunaamini Muungano huu ni muhimu
ukadumishwa na kuimarishwa. CCM tunaaamini ili Muungano huu udumu njia
pekee kwasasa ni kufanya marekebisho kwenye Muundo wa serikali mbili ili
ujibu vizuri zaidi changamoto mbalimbali zilizoibuliwa na kukidhi
mazingira ya sasa.
Tunawaomba wanaCCM na watanzania kwa ujumla kuwa watulivu katika kipindi
hiki. Ni vizuri Watanzania tukavumiliana,tukashindana kwa hoja
tukitanguliza mbele uzalendo na masilahi ya kweli ya nchi yetu.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
Imetolewa na;-
Nape Moses Nnauye
Katibu wa Itikadi na Uenezi
20/03/2014
0 comments:
Post a Comment