Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Aprili mwaka uliopita, Jeshi la Polisi lilitangaza kwamba lingerudisha
utaratibu wa kuajiri vijana kutoka shuleni ili ‘kukidhi mahitaji ya
sasa’ ya jeshi hilo.
Tumeguswa mno na hatua ya Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar
es Salaam ya kuwafukuza kazi askari wake wanne kwa kushirikiana na
majambazi kufanya uhalifu. Askari hao walifukuzwa kazi baada ya
kuthibitika kwamba Machi 9, mwaka huu walishirikiana na majambazi 11
kupora kwa kutumia silaha katika ofisi ya Hong Yang inayojihusisha na
shughuli za ujenzi na useremala iliyoko Mbezi Beach, jijini Dar es
Salaam.
Tunasema tumeguswa mno na hatua hiyo kutokana na
jeshi hilo, kwa muda mrefu, limeshindwa kuwang’amua na kuwatimua askari
wanaoshirikiana na majambazi kufanya uhalifu, licha ya kelele na
malalamiko kutoka kwa wananchi kwamba matukio mengi ya ujambazi
yanahusisha baadhi ya askari wa jeshi hilo. Kelele za wananchi pia
zimekuwa zikielekezwa kwa jeshi hilo kutokana na askari wake wa ngazi
mbalimbali kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Tunaunga mkono hatua ya kuwatimua askari hao kwa
sababu siyo tu wamefanya uhalifu, bali pia vitendo vyao kwa namna moja
ama nyingine vimelidhalilisha Jeshi la Polisi, mbali na kuwakwaza askari
ambao ni waadilifu, watiifu na waaminifu wanaotekeleza majukumu yao
kikamilifu. Siyo siri kwamba taswira ya jeshi hilo imechafuliwa kwa
kiasi kikubwa na askari wake wanaoendekeza tamaa za kupata utajiri wa
harakaharaka, huku wakiweka kando viapo vyao na maadili ya kazi yao.
Ndio maana wananchi wamechoshwa na vitendo vya askari hao na wanataka
kuona wakitimuliwa na kufunguliwa mashtaka.
Tatizo tunaloliona hapa ni mfumo mbovu wa kutoa
ajira kwenye jeshi hilo. Utaratibu mzuri uliozoeleka zamani wa kuchuja
vijana wakiwa bado shuleni umewekwa kando kwa sababu zisizoeleweka.
Badala yake wanaajiriwa vijana bila ya kujua historia yao na wengine
wakiwa wa wanatoka kwenye mazingira ya kihalifu. Wengine wanaajiriwa kwa
misingi ya rushwa na ‘undugu’, wakati wengine wanaingizwa kwa kuwa
watoto wa wakubwa. Hicho ndicho kiini cha kansa inayolitafuna Jeshi la
Polisi hivi sasa.
Tuliwahi kushauri kwamba ajira katika jeshi hilo
zisitolewe kiholela, bali zitolewe kwa vijana waliofaulu kidato cha sita
au wenye shahada za vyuo vikuu waliopata mafunzo ya Jeshi la Kujenga
Taifa (JKT). Hoja yetu ya msingi ilikuwa kwamba vijana wa aina hiyo siyo
tu wanakuwa wamepikwa na kufundwa, bali pia wanakuwa wamechunguzwa na
kuonekana wana nidhamu inayotakiwa katika majeshi yetu.
Aprili mwaka uliopita, Jeshi la Polisi lilitangaza
kwamba lingerudisha utaratibu wa kuajiri vijana kutoka shuleni ili
‘kukidhi mahitaji ya sasa’ ya jeshi hilo. Uamuzi huo ulitokana na jeshi
hilo kutambua changamoto zinazolikabili kutokana na maendeleo ya sayansi
na teknolojia, ikiwa ni pamoja na ongezeko la uhalifu mpya kama wizi wa
kutumia mtandao, biashara ya dawa za kulevya, usafirishaji haramu wa
binadamu na utakasaji wa fedha. Lilitambua pia kwamba sasa wahalifu
wanatumia mbinu mpya na utaalamu wa hali ya juu.
Tulilipongeza jeshi hilo kwa kujitambua, lakini
tulipendekeza yafanyike maboresho ili kuliwezesha kuwa jeshi la kisasa
siyo tu litakaloweza kuvutia vijana wenye ari, weledi, utashi na dhamira
ya kufanya kazi za Polisi, bali pia vijana wenye mtazamo na mwelekeo
unaoendana na dunia ya sasa. Kinachosubiriwa hadi leo ni utekelezaji wa
azma hiyo.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment