Home » » Sakata la kampeni za kuwania urais 2015 lazidi kuibua mapya CCM

Sakata la kampeni za kuwania urais 2015 lazidi kuibua mapya CCM

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Siku nne baada ya Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye kueleza kuwa amekata rufaa Kamati Kuu (CCM) kupinga adhabu ya onyo aliyopewa kwa kuanza mapema kampeni za urais, wenzake watano waliokumbwa pia na adhabu hiyo wamesita kufanya hivyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi yao walidai hawajapewa barua za onyo kwa kudaiwa kufanya kampeni za urais wa 2015 kabla ya muda wake.
Sumaye na wanachama wenzake, Edward Lowassa, Bernard Membe, Stephen Wassira, William Ngeleja na January Makamba walitiwa hatiani kwa kuanza kampeni mapema, hivyo kupewa onyo linalokwenda sambamba na kutowania nafasi yoyote ndani ya chama kwa miezi 12.
Hata hivyo, juzi Sumaye alipotakiwa na gazeti hili kueleza alikata rufaa hiyo kwa kutumia kanuni ipi, alisema mpaka sasa hajapata mrejesho wowote kwa sababu kanuni hazielezi ni muda gani anatakiwa kuwa amepewa taarifa kuhusu rufaa hiyo.
Kauli hiyo ya Sumaye ilipingwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye ambaye alisema mwanachama yeyote lazima akate rufaa kwa kutumia kifungu cha kanuni husika, ili ajue rufaa yake itasikilizwa ngazi ipi ya uongozi.
Makamba ambaye ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia alisema atatoa msimamo wake kama atakata rufaa ama la, baada ya kupokea barua inayoonyesha tuhuma zinazomkabili ndani ya CCM.
Kamati Ndogo ya Nidhamu inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Philip Mangula ndiyo iliyowatia hatiani vigogo hao ambao wote kwa pamoja wamekuwa wakidaiwa kuutaka urais.
Akizungumza na gazeti hili katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma jana, Makamba alisema hadi sasa hajapokea barua kutoka ndani ya chama inayoonyesha anachotuhumiwa.
“Sijui yeye (Sumaye) amepata barua ya kumwonyesha anachotuhumiwa, mimi sijapewa barua kwa hiyo siwezi kusema kuhusiana na uamuzi nitakaochukua,” alisema Makamba na kuongeza;
“Hayo ni maneno tu ya magazeti, kimsingi sina ninachotuhumiwa, magazeti yaliandika Makamba amwaga pikipiki kwa waendesha bodaboda Mwanza, kimsingi nilichofanya pale ni kuwaunganisha waendesha bodaboda na kampuni inayouza pikipiki hizo, mimi sikulipa fedha zangu.”
Wassira alipoulizwa iwapo atakata rufaa kuhusu uamuzi huo alisema; “Nimekubali yaishe.”
Kwa upande wake, Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa kupitia msaidizi wake, alisema hana maoni kuhusiana na uamuzi huo.
Naye Mbunge wa Sengerema na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, alikataa kuzungumzia jambo hilo kwa madai kuwa yeye siyo msemaji wa chama.
“Mimi siyo msemaji wa chama. Kama unavyofahamu chama chetu kina wasemaji wake ambao ndiyo wanaotakiwa kuzungumzia mambo hayo,” alisema Ngeleja.
Februari 20 mwaka huu, Membe aliipongeza CCM kwa kuwapa adhabu wasaka urais akiwamo yeye mwenyewe na kusisitiza kuwa kila chama lazima kifuate utaratibu wa kupata viongozi wake.
Chanzo;mwananchi

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa