Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Umeibuka ulevi mpya nchini ambao umethibitika kuwateka vijana
hasa wa jiji la Dar es Salaam, huku kukiwa na taarifa za kitaalamu
kwamba ulevi huo una athari za kiafya kwa watumiaji.
Ulevi huo ni kupitia starehe au anasa mpya ya
uvutaji shisha; ulevi ambao watengenezaji hutumia chombo maalumu chenye
bomba la kutolea moshi, ambacho huwekwa tumbaku, maji na moto.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa
tumbaku huwekwa katika chombo hicho na kuunguzwa kwa moto, kisha moshi
wa tumbaku hupita kwenye maji na huingia kwenye bomba, kisha watumiaji
huanza kuvuta.
Sehemu maarufu ambako shisha inauzwa ni Ufukwe wa
Coco, maeneo ya Kinondoni, Mwananyamala, Sinza Barabara ya Shekilango na
maeneo kadhaa ya mitaa ya mjini.
Mmoja wa watumiaji wa shisha, Ismail Ndunguru
alisema yeye na vijana wenzake hutumia siku za mwisho wa wiki kwenda
kuburudika kwa uvutaji katika hoteli moja iliyopo mjini, Mtaa wa Garden
jijini Dar es Salaam.
“Kuvuta shisha kwa siku nzima ni Shilingi 10,000,
mkimaliza, mnarudisha bomba. Tukiwa vijana wengi inafurahisha sana
kuvuta,” alisema Ndunguru.
Taarifa za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaeleza
kuwa, mkupuo mmoja wa shisha, una kemikali hai 4,800 na kwamba kemikali
hizo husababisha saratani ya mapafu, maradhi ya moyo na maradhi ya
mfumo wa upumuaji.
WHO inaeleza kuwa, kiasi cha uvutaji wa shisha kwa saa moja ni sawa na kuvuta sigara 100 au 200.
Daktari Bingwa wa magonjwa ya ndani ya mwili na
mfumo wa hewa, Meshack Shimwela alisema madhara ya shisha ni kama yale
yanayosababishwa na uvutaji wa sigara pengine na zaidi kutokana na
kilevi hicho kuwa na tumbaku nyingi.
Dk Shimwela alisema licha ya kuwa watengenezaji na
wavutaji wa shisha hudai kuwa haina madhara kwa sababu huchanganywa na
maji, lakini bado madhara yake ni makubwa.
“Maradhi yote yanayosababishwa na uvutaji wa
sigara ndiyo yanayosababishwa na shisha, kwa mfano saratani ya mapafu na
mdomo, kifua kikuu na mzio ambao unaweza kusababisha pumu,” alisema Dk.
Shimwela.
Dk. Shimwela alisema ni vizuri watumiaji wakajua
madhara ya shisha, badala ya kuchukulia kuwa ni mtindo wa maisha tu au
starehe isiyo na madhara.
Hivi karibuni, Profesa Twalib Ngoma, Mkurugenzi wa Taasisi ya
Saratani ya Ocean Road, alisema asilimia 40 ya saratani zote nchini
zinasababishwa na matumizi ya tumbaku.
Biashara inavyofanyika
Shisha inauzwa katika sehemu kadhaa za starehe za
Jiji la Dar es Salaam kwa sasa na maeneo yanayouza bidhaa hiyo
yanafahamika kama ‘shisha lounge au shisha point’.
Mwandishi wa Mwananchi akiambatana na Ndunguru
walikwenda hadi Kinondoni katika hoteli moja ambako wavutaji wa shisha
walikuwa wakiendelea ‘kuburudika’ huku wakipuliza moshi hewani.
Waliitozwa Sh15,000 kisha nao waliletewa chombo
cha kuvutia. Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa unaonyesha kuwa bei ya
shisha hutegemea sehemu inapouzwa, hivyo huuzwa kati Sh10,000 na 70,000.
Ndunguru alisema shisha haina madhara kwake ingawa
alipovuta kwa mara ya kwanza, alikohoa sana lakini sasa anaiona kuwa
kiburudisho kinachompa faraja kama wavutaji wa sigara na kwamba hamu ya
kuvuta kila mara imeingia mwilini mwake.
Ilibainika kuwa kwenye shisha huwekwa ladha kadhaa
kama vile vanila, strawberry, mint, chocolate au kahawa ili kuwavutia
wavutaji. Ladha hizo zinatajwa kuwa kivutio cha mabinti ambao wameingia
kwa kasi kwenye uvutaji huo.
Kadhalika uchunguzi ulibaini kwamba wanafunzi wa
shule za sekondari na vyuo vikuu, kwa makundi hujikusanya na kuchanga
fedha kwa ajili ya kuvuta shisha.
Habari zaidi zinadai kuwa wafanyabiashara wa
shisha hivi sasa wanachanganya dawa za kulevya kama heroin na bangi
katika shisha kama kivutio kwa watumiaji.
“Hii ni biashara kubwa sana sasa hivi, kwa siku
moja, mimi naingiza zaidi ya Sh150,000 kwa kuuza bomba la shisha,”
anasema mfanyabiashara mmoja wa Kinondoni.
Muuzaji wa shisha katika eneo la Coco Beach, Said
Coco alisema biashara hiyo ni nzuri na kwamba wateja wamekuwa
wakiongezeka kadiri kila siku.
Coco alisema wateja wake wakubwa ni vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 40 ambao huvuta shisha kila mwishoni mwa wiki.
Hata hivyo, alikanusha habari kwamba wafanyabiashara wanaweka
dawa za kulevya na bangi kwenye shisha, ingawa anasema kama wapo
wanaofanya hivyo basi wanaharibu starehe hiyo ambayo yeye anasema haina
madhara.
Serikali inasemaje?
Waziri wa Afya, Dk Seif Rashid alisema anafahamu
kuwa shisha imepata umaarufu nchini hususan Dar es Salaam, lakini ni
vigumu kuwakamata watumiaji.
Alisema wizara haiungi mkono matumizi ya shisha kwani inafahamu kuwa ni kilevi hatari pengine kuliko sigara za kawaida na pombe.
“Shisha ni hatari na sisi hatuungi mkono, lakini
hatuwezi kuwakamata watumiaji kama ambavyo hatuwezi kuwakamata walevi wa
sigara na pombe. Lakini tunawaasa watengenezaji wa shisha kuweka nembo
ionyeshayo kuwa ni kilevi hatari,” anasema.
Dk. Rashid alisema matumizi ya tumbaku
yanasababisha maradhi mengine hasa saratani ambayo inasababisha
kiharusi, maradhi ya moyo na ngozi.
Kwa upande wake Kamishna wa Polisi Kitengo cha
Kupambana na Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa alisema hana taarifa za
ongezeko la matumizi ya shisha nchini, ingawa aliwahi kuona kilevi hicho
nchini Misri.
Nzowa alisema ikiwa itagundulika kuwa shisha ina
wingi wa Nicotine, atachukua hatua kali dhidi ya wahusika, huku akitoa
mfano wa kilevi cha kuber kilichowahi kupigwa marufuku.
Asili ya shisha
Shisha ni jina lenye asili ya Misri (sheesha) lenye maana ya bomba la maji lililounganishwa kwenye kontena.
Tumbaku iliyochanganywa na ladha ya matunda,
hujazwa kwenye chombo mfano wa chetezo, moto huwekwa kati na sehemu moja
huwekwa maji.
Moshi wenye harufu au ladha hutoka kupitia bomba hilo na kuvutwa.
Mvutaji huvuta kwa kutumia bomba (huweza kuwa la plastiki) na mabomba mengine yanaweza kutumiwa na kutupwa (disposable).
Athari zake kiafya
Kuharibu ogani; Shisha inatajwa kuwa na hewa ya
carbon monoxide ambayo huingia kwenye mapafu na kuchukua nafasi ya hewa
safi ya oxygen, hivyo ogani muhimu kuharibika.
Saratani; Shisha ina wingi wa nicotine, kiwango
cha kemikali za tar, carbon monoxide, metali za kiwango cha juu kama
cobalt na lead ambavyo ni visababishi vya saratani.
Utegemezi (adiction); Uvutaji wa shisha
husababisha kutengenezwa kwa kiwango kikubwa cha nicotine kwenye damu,
hivyo mtu akishazoea kuvuta hawezi kuacha kwani kilichomo kwenye shisha
huvutwa kwenye neva za fahamu na kusababisha mishipa hiyo kwenye ubongo
kuhisi kupata faraja na raha ya kipekee.
Maradhi ya kuambukiza; Uvutaji wa shisha hutumia
bomba ambalo watu kadhaa hushirikiana. Hali hii husababisha maradhi ya
kuambukiza kama Kifua Kikuu (TB) na hepatitis B (homa ya ini).
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment