Home » » Uongozi wa mtaa walalamikiwa kwa migogoro ya ardhi Dar

Uongozi wa mtaa walalamikiwa kwa migogoro ya ardhi Dar

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Prof. Anna Tibaijuka
 
Baadhi ya wakazi wa Kata ya Mbezi Makabe, Dar es Salaam, wameulalamikia uongozi wa serikali ya mtaa kuwa chanzo cha migogoro ya ardhi.
Wamesema uongozi huo umekuwa ukiuza ardhi kwa zaidi ya mtu mmoja hasa baada ya wamiliki wa awali kufariki dunia.

Flora Mwingira, msimamizi wa mirathi ya familia ya Venance Mwingira baada ya baba yake kufariki dunia mwaka 2005, amdai mwenyekiti wa mtaa, Zuberi Zahoro, aliwazunguka watoto wa marehemu na kugawa ardhi yao kwa Aloyce Massawe ambaye kwa sasa ni marehemu.

Alisema Masswe aliyefariki dunia 2012, toka enzi za uhai wa baba yake (Mwingira) alikuwa akitaka kununua shamba lao, lakini alikatataliwa mara zote kwa madai ya kuwa hiyo ilikuwa mali ya watoto wa Mwingira.

“Baba yetu alikuwa akitupatia taarifa za Massawe kumg’ang’aniza auziwe shamba,  lakini ikashindikana. Baada ya kusikia baba yetu amefariki, Massawe akaanza kushirikiana na serikali ya mtaa kudai tuachie eno hilo kwani aliuziwa na baba,” alisema na kuongeza: “Cha kushamgaza ni kwamba hata Massawe alipofariki dunia Zahoro ametuletea wamiliki wapya wakidai hao ni warithi wa Massawe.”

Mjumbe wa zamani wa shina, ambaye pia alikuwa shahidi wakati Mwingira ananunua shamba hilo mwaka 1985, Ally Hassan, alisema anachotambua yeye ni kwamba shamba ni mali ya Mwingira.

Hassan alidai Massawe aliwahi kumfuata na kumwambia amtambue kama mmiliki mpya wa shamba la Mwingira, lakini alipokuwa akimwambia aende na muuzaji (Mwingira) kwake ili athibitishe kumuuzia shamba, Massawe alishindwa kulitekeleza hilo.

“Baada ya kuzongwa sana ilifika wakati nikamuuliza Mwingira mwenyewe kuhusu madai ya Massawe na kujibu kwamba hakuna kitu kama hicho. Aliniambia mauziano yaliposhindikana Massawe aliomba apewe eneo kwa ajili ya kulima tu, lakini mwenye mali alikataa kwa hofu ya kudhulumiwa,” alisema Hassan.

Mjumbe wa shina wa sasa, Betty Mbena, alithibitisha kupokea wageni waliodai kuwa ni ndugu wa Massawe na kutaka waonyeshwe eneo la ndugu yao, lakini alikataa kwa kuwa vielelezo alivyokabidhiwa na mjumbe mstaafu vinaonesha  mmiliki ni Mwingira.

Alisema ujio wa wageni hao wanne wakiwemo wanajeshi ulikuwa wa vitisho na kuwa baada ya mjumbe kugoma kuwaonyesha eneo, waliamua kumuita askari polisi, kutoka kituo cha polisi cha Mbezi kwa Yusuph ili kumkamata mmoja wa wamiliki wa eneo hilo aliyekuwepo kwa mjumbe muda ule.

Alisema baada ya kuona vurugu, wanajeshi hao waliondoka na kurudi baada ya siku chache, wakiwa wameongozana na mjumbe wa serikali za mtaa na mtu mwingine waliyedai kwamba wanataka kumuuzia eneo hilo.

“Sikuwahi kumuona ndugu yeyote wa Massawe kwani alikuwa mara zote akija peke yake. Sasa nashangaa hao ndugu wametoka wapi tena hata bila ya ushahidi wowote wa kuonyesha kuwa eneo ni la ndugu yao,” alieleza Betty.

Kwa mujibu wa Flora, baada ya vurugu familia ya Mwingira iliongozana na mjumbe huyo hadi serikali za mtaa na kuelezwa kwamba kutokana na mjumbe kukataa kuweka sahihi ya mauziano, uongozi wa mtaa uliuza eneo lao kwa mnunuzi yule yule aliyepelekwa na waliodai kuwa ndugu wa Massawe.

Akijibu madai hayo Mwenyekiti Zahoro alisema anachotambua ni kwamba eneo sio la Mwingira kwani siku chache kabla ya Masawe kufariki aliitwa katika Mahakama ya Mwanzo Sinza na kuelezwa kwamba eneo ni la Massawe na ndugu zake wameshagawana.

Awali, alithibitisha kuwa vielelezo vyote kama mwenyekiti wa mtaa, vinavyoonesha kuwa mmiliki ni Massawe anavyo na alihaidi kuvionyesha, lakini hakufanya hivyo.

Alisema Massawe alisimama na Mwingira mahakamani mwaka 2012 na kushinda kesi, lakini mwenyekiti alipoombwa kueleza Mwingira alisimamaje mahakamani wakati alishafariki zaidi ya miaka saba nyuma, alisema mahakama ndiyo inayoweza kujibu swali hilo.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa